MARA kwa mara kumekuwa na taarifa za ufujaji na wizi wa mabilioni ya shilingi katika taasisi na idara za serikali unaofanywa na baadhi ya watendaji waliopewa dhamana ya kusimamia fedha hizo kwa ajili ya maendeleo kwenye sekta mbalimbali.
Taarifa hizo zimekuwa zikibainisha kwamba fedha hizo zinazopigwa na watendaji hao ni zile zinazotolewa na serikali kuu na za mapato ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi kama vile ya elimu, afya na miundombinu.
Fedha zingine ni zile zinazotokana na ukusanyaji wa ushuru katika minada, masoko na mialo na ubadhirifu huo hufanya na watendaji wa halmashauri kwa kushirikiana na wazabuni.
Ubadhirifu au upigaji wa fedha za umma umekuwa ukidaiwa kufanywa na watendaji wa taasisi kwa kushirikiana na wazabuni. Katika eneo hilo, baadhi ya zabuni hutolewa kwa misingi ya upendeleo lengo likiwa kujipatia chochote kupitia fedha za utekelezaji wa kazi mbalimbali kama ujenzi wa miundombinu ya barabara, afya, maji na elimu.
Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Kamati za Kudumu za Bunge, Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) zimekuwa zikibainisha mara kwa mara upigaji unaofanywa na watendaji hao. Ripoti hizo zimekuwa zikijirudia kila mwaka lakini hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa ili kukomesha vitendo hivyo visiendelee.
Aidha, kila viongozi wakuu wa serikali, kwa maana ya Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Naibu Waziri Mkuu wanapofanya ziara katika mikoa kukagua shughuli za maendeleo, wamekuwa wakikutana na madudu hayo ambayo yamesababisha mabilioni ya fedha za umma kuingia katika mifuko ya wajanja wachache.
Matokeo ya kuendelea kwa vitendo hivyo ni kukithiri kwa ubadhirifu wa fedha za umma na hatimaye kuzorotesha miradi mbalimbali ya maendeleo. Kwa mantiki hiyo, kero zinazowakabili wananchi zimekuwa zikiendelea kuwapo huku yakitolewa maagizo ya kusimamishwa kazi kwa watuhumiwa ili kupisha uchunguzi kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
Pamoja na kuwapo kwa ushauri wa CAG kuhusu hatua za kuchukua dhidi ya waliohusika na ubadhirifu pamoja na maagizo yanayotolewa na viongozi hao, utekelezaji wa hatua hizo ikiwamo uchunguzi wa TAKUKURU, hatua zinazochukuliwa hazikidhi kiu ya wananchi kuona wahusika wanafikishwa katika vyombo vya sheria na kuadhibiwa.
Kuwapo kwa hali hiyo, kunafanya misamiati ya ubadhirifu, wizi na upigaji kuwa kama aya ndani ya misahafu na kuwafanya baadhi ya watumishi pia kuona ni mfumo wa kawaida ulioko katika maisha, hivyo wapigaji wa mabilioni hayo kuonekana ndio mashujaa na wale wanaofuata maadili kuwa kama waliozubaa.
Kuibuliwa kwa madudu hayo, ni dhahiri kwamba chanzo kikuu ni kukosekana kwa usimamizi imara wa fedha hizo unaopaswa kufanywa na wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na watendaji wakuu wa wizara. Kwa hali ya kinadharia, kuendelea kwa hali hiyo kunaweza kuitafsiriwa kuwa kuna mnyororo wa ushirikiano katika ngazi mbalimbali ambao pia kusababisha watu kulindana.
Maneno na hadithi za upigaji mabilioni ya fedha za hauna budi kufika mwisho kwa serikali kuchukua hatua. Njia inayoweza kufanikisha hilo ni kuimarisha uwajibikaji kwa watendaji.
Iwapo kutatokea ubadhirifu katika sekta fulani na sehemu husika, waliohusika wakawajibishwa sambamba na mkuu wa wilaya, mkurugenzi wa halmashauri, katibu tawala wa mikoa na hata waziri wa kisekta, ni wazi kwamba kila mtu atajifunza kusimamia mali za umma kwa kuhofia kupoteza kazi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED