WAFANYABIASHARA wa vipodozi wanajukumu kubwa kuhakikisha wateja wao wanakuwa salama kwa kutumia bidhaa wanazouza bila kupata madhara.
Lakini baadhi yao wamekuwa wakiingiza vipodozi vyenye viambata vya sumu na kusababisha watu kuharibika ngozi na hatimaye kupata magonjwa ya saratani.
Pamoja na serikali kupiga marufuku uingizaji wa bidhaa za vipodozi vyenye viambata vya sumu, lakini baadhi ya wafanyabiashara hao hutumia njia za panya kuziingiza nchini.
Hata uuzaji wake huwa ni wa siri na wanaowauzia ni wateja wao waliowazoea.
Kuna maduka katika baadhi ya sehemu hufunguliwa nyakati za usiku pekee ili kuuza vipodozi hivyo na wateja wao wanayajua yalipo.
Hii ni hatari kwa sababu wananchi wanaendelea kuathirika kwa kukosa uelewa wa kutumia bidhaa hizo zilizopigwa marufuku.
Katika kukabiliana na suala hilo, Shirika la Viwango Nchini (TBS), limewataka watu wote wanaofanyabiashara ya chakula na vipodozi kusajili maeneo yao ili iwe rahisi kukaguliwa kwa ajili ya usalama wa afya za wananchi.
Vile vile, shirika limewataka wafanyabiashara na watumiaji wa bidhaa kuhakikisha bidhaa wanazonunua zina nembo ya alama ya ubora.
TBS imesisitiza kuwa wanaofanyabiashara ya vipodozi wanapaswa kuhakikisha vipodozi hivyo havina viambata sumu vyenye madhara kwa afya za watumiaji.
Watumiaji wa vipodozi hivyo mara nyingi hupenda kubadili ngozi zao na kutaka kufanana na watu weupe bila kujua athari zake.
Wengi wanaotumia baadaye ngozi zao hupata madhara kiasi cha kushindwa kutembea kwenye jua kwa sababu ngozi zao zinakuwa zimeshaathirika.
Wengine hulazimika kutembea na miamvuli kujikinga na jua lisipenye moja kwa moja kwenye ngozi zao.
Madhara ya vipodozi hivyo pia ni ngozi kuungua na badala ya kupata rangi wanayoitaka huwa wekundu na hatimaye weusi kama rangi ya mkaa.
Pamoja na elimu ya kuwataka wananchi kuacha kutumia vipodozi vyenye viambata vya sumu, lakini ni kama inawashawishi kuendelea kutumia kwa kutaka kubadili ngozi waliyozaliwa nayo na kuiga rangi za watu weupe.
Mara kwa mara tumeshuhudia TBS ikiteketeza tani kwa tani za vipodozi vyenye viambata vya sumu, lakini wafanyabishara wanaendelea kuviingiza na kuangamiza maisha ya wananchi wenzao.
Na kwa wanaotumia bidhaa hizo wakumbuke kuwa urembo sio mtu kuwa mweupe, hata hao wenye rangi nyeupe wanatamani wawe weusi, lakini wanashindwa wataipataje.
Ndio maana hao wanaoonekana kuwa warembo kwa sababu ya rangi zao nyeupe, wanajianika kwenye jua ili wapate rangi nyeusi.
Ni lazima kabla ya kuiga kitu mtu afahamu faida na hasara zake kabla ya kuamua kukifanya.
TBS ina kazi kubwa ya kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye maduka yanayouza vipodozi ili kuwabaini wanaoendelea kuviingiza.
Na wenye viwanda vinavyozalisha bidhaa hizo pia wanapaswa kukaguliwa ili kujiridhisha wanazalisha kwa ubora unaotakiwa.
Kuthibitisha ubora wa bidhaa wanazozalisha na mifumo ya kimenejimenti na kusajili bidhaa za chakula na vipodozi.
Wanunuzi wa bidhaa hizo pia wanatakiwa kuthibitisha kuwa zina nembo ya uhakiki wa TBS ili kuwa na uhakika kwamba ni yenye ubora na ikitumiwa haileti madhara kwa mtumiaji.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED