RIPOTI MAALUM: Taharuki wazazi na wanafunzi shule kufungwa zaidi ya mwaka

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:28 AM Dec 21 2024
Shule ya Awali na Msingi ya Rainbow iliyoko Toangoma.
Picha:Mpigapicha Wetu
Shule ya Awali na Msingi ya Rainbow iliyoko Toangoma.

SHULE inafungwa kwa mwaka mmoja na nusu, kupisha ujenzi. Zaidi ya wanafunzi 600, kuanzia darasa la awali hadi la saba wa shule hiyo, sasa hawana pa kusomea.

Hii ni Shule ya Awali na Msingi ya Rainbow iliyoko Toangoma, Kigamboni mkoani Dar es Salaam. Inamilikiwa na Kanisa la Tanzania Presbyterian (TPC) ikiwa na namba za usajili: PS 0206136 na ilianza kutoa huduma mwaka 2011.

Taarifa za kufungwa kwa shule hiyo zimethibitishwa na wazazi na walezi wa wanafunzi ambao Desemba 6, mwaka huu, walitumiwa ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) na uongozi wa shule. Ujumbe huo ulikuwa unawaarifu kwamba shule inafungwa kwa mwaka mmoja na nusu kuanzia Januari Mosi, 2025, hivyo watafute shule zingine kwa ajili ya watoto wao.

Mwandishi wa habari hii ameona ujumbe huo wenye maneno 155, kisha kumtafuta Meneja wa Shule, Mchungaji Hallington Kamanga, ambaye amekiri kuutuma kwa wazazi. 

Ujumbe huo umetumwa kipindi ambacho shule zimekwishafungwa na usaili wa wanafunzi umeshafanyika kwenye shule nyingi. Licha ya kutangaza kuifunga shule hiyo, Mchungaji Kamanga hajaeleza hatima ya kimasomo kwa wanafunzi waliokuwa wakisoma shuleni hapo.

USEMAVYO UJUMBE 
Ujumbe mfupi wa Mchungaji Kamanga uliotumwa kwa wazazi na walezi,  ambao Nipashe imefanikiwa kuuona unasema: “Ndugu Mzazi/Mlezi, Shalom!  Uongozi wa Kanisa la TPC umepokea Shule ya Rainbow mnamo 03/10/2024, ikiwa na idadi ndogo sana ya wanafunzi inayopelekea kukosa sifa ya kuwa kituo cha mtihani mwakani 2025. 

“Kwa sababu hiyo, kanisa limekusudia kuanza na uboreshaji wa mazingira; kubomoa madarasa yaliyopoteza hadhi kwa kutofanyiwa maboresho kwa muda mrefu, na kujenga majengo mapya katika mfumo wa ghorofa.

  “Tunapendekeza kusitisha masomo kwa madarasa ya elimu ya msingi kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu kupisha ujenzi na hivyo kukuomba wewe mzazi umtafutie mwanao shule nyingine. 

“Ujenzi utakapokuwa umekamilika tutapokea wanafunzi tena na kuendelea na huduma ya elimu. Kwa kuwa wayajua vema mazingira ya shule jinsi yalivyo, tunatumai kuwa utaona umuhimu wa kile kinachokusudiwa kufanyika ili kuongeza hadhi, ubora  na thamani ya shule kwa manufaa ya sasa na ya wakati ujao. 

“Wanafunzi wa Chekechea (Pre-Primary) wataendelea na masomo.  Wizara ya Elimu tayari imethibitisha jina jipya la  shule na meneja tangu 19/11/2024. Sasa shule inaitwa "HEPHZIBAH PRE & PRIMARY SCHOOL.”

Alipoulizwa sababu za kutoitisha kikao cha wazazi badala ya kutuma ujumbe huo, Mchungaji Kamanga anasema, hawezi kutoa ufafanuzi kwa kuwa jambo hilo limekuwa mahakamani kwa muda mrefu.

TAHARUKI WAZAZI
Kutokana na hali hiyo, sintofahamu imeibuka kwa wazazi na walezi ambao wamelalamikia uongozi wa shule kutoitisha kikao rasmi, jambo linalohusu hatima ya wanafunzi kielimu.

Baadhi ya wazazi wenye watoto shuleni hapo wameliambia gazeti hili kwamba baada ya kutumiwa ujumbe huo, waliomba kuonana na uongozi wa shule bila mafanikio.

Mama mwenye watoto wawili shuleni hapo, Magreth Kamaghe, anasema lengo la wazazi kuomba kuonana na uongozi ni kupata suluhu itakayowasaidia watoto wasiathirike kimasomo.

Anasema kabla ya ujumbe wa Mchungaji Kamanga, Septemba, mwaka huu walisikia tetesi za shule hiyo kufungwa lakini walipofuatilia kwa nyakati tofauti, uongozi wa shule na wa kanisa ulikanusha na kudai ni uzushi, huku wakiwataka waupuuze.

“Badala yake walituambia wanabadilisha menejimenti kwa kuleta nyingine mpya, lakini shule itaendelea kama kawaida. Kweli baada ya shule kufunguliwa ile Septemba, waliitisha kikao cha dharura na kuleta uongozi mpya, ambao ulituhakikishia kuwa shule haitafungwa,” anasema.

Mzazi mwingine, Dk. Sixberth Mlowe, anasema wameshtushwa na uamuzi huo wa ghafla, licha ya kwamba wazazi na walezi walikuwa wanawasiliana na uongozi kila waliposikia tetesi.

“Ni uamuzi wa kikatili kwa watoto na wazazi. Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba shule hii inamilikiwa na kanisa ambalo lina shule zingine za msingi, hawajataka kujali na kuwaza kuwahamishia watoto kwenye shule hizo nyingine, badala yake wameamua kuwafukuza,” anasema.

Dk. Mlowe ameiomba serikali iingilie kati ili kunusuru hatima ya wanafunzi hao kielimu.
“Tunaona haya yanafanyika pengine kwa sababu wamiliki wa hii shule sio Watanzania, ni raia wa kigeni, lakini wanaoumia ni kizazi cha Tanzania.

“Kufukuza mtoto wa darasa la kwanza bila huruma ni kutojali taifa la kesho. Tunaiomba serikali iangalie kwa jicho la ziada ukatili huu, ili watoto hawa wasio na hatia, wapate haki yao ya elimu,” anasema

Alipoulizwa kuhusu uamuzi wa ghafla wa kuifunga shule, Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Dennis Mbiro, anasema yeye si msemaji wa suala hilo, bali uongozi wa kanisa kwa kuwa alikuwa anakaimu kwa kipindi cha mpito.

MKURUGENZI WA SHULE
Nipashe ilipomtafuta Mkurugenzi wa Shule za TPC, Pius Balihuta, kuzungumzia suala hilo, anasema uamuzi huo umefikiwa baada ya uongozi wa kanisa kushinda kesi iliyokuwa imefunguliwa na mchungaji aliyekuwa anasimamia shule hiyo.

“Mmishionari aliyepewa aisimamie alitaka aitoe kwenye umiliki wa kanisa ili iwe mali yake binafsi. Shauri likafunguliwa mahakamani ambako kanisa lilishinda kesi na kurudishiwa shule,” anafafanua.

Anasema kesi hiyo ya madai namba 28/2022, ilifunguliwa na wachungaji Jung Hwan Kim na Sang Ok Nam, waliokuwa walalamikaji dhidi ya Bodi ya Wadhamini ya TPC waliokuwa washtakiwa.

Nakala ya hukumu ya kesi hiyo, ambayo Nipashe imeiona, ilitolewa Februari 5, mwaka huu, na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, John Nkwabi. Katika kesi hiyo, upande wa walalamikaji uliwakilishwa na Wakili Hamis Mbangwa na walalamikiwa uliwakilishwa na Wakili Paschal Kamala.

Hata hivyo, anasema licha ya mahakama kuirejesha shule kwenye uongozi wa kanisa mapema mwaka huu, uongozi wa kanisa haukuichukua shule hadi Septemba, mwaka huu.

“Kanisa limekuja na shauri moja la kuwaomba wazazi kama wataweza kuwahamisha watoto ili lifanye ujenzi mpya kwa maana ya kuvunja baadhi ya majengo na kujenga yanayofaa. Hatujawafukuza kwa sababu bado hatujafikia mwafaka,” anasema.

 Balihuta anasema hajaafiki ombi la wazazi la kuhamisha wanafunzi hao moja kwa moja kwenda shule nyingine ya TPC na badala yake, wameelekeza wafanye maombi ya kuhamia na kufanya usaili.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, utaratibu wa TPC ni kuchukua wale watakaofaulu mitihani ya usaili na si vinginevyo.
“Tumewaomba hao wazazi wawatafutie watoto shule zingine kwa mwaka mmoja na nusu, ili tufanye maboresho ya shule na baada ya hapo tutangaze kutafuta wanafunzi. Watakaofaulu ndio tutawachukua.

“Mzazi ambaye ataona ni sawa mtoto kusoma ujenzi ukiendelea, sisi tutamfundisha. Hatujawafukuza,” anasema.

SHULE NYINGINE
Uchunguzi wa Nipashe umebaini kwamba, miezi minane ya TPC kutoingiza menejimenti mpya shuleni Rainbow sasa Hephzibah, ulilenga kuwawezesha walalamikaji, Jung Hwan Kim na Sang Ok Nam, kujenga shule mpya.

Mmoja wa wazazi mwenye wanafunzi shuleni hapo, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, anadai kilichotokea ni hujuma dhidi ya kizazi cha Tanzania.

Anasema TPC ilishirikiana na menejimenti ya zamani kuwezesha ujenzi wa shule mpya katika eneo la Kisarawe II, lililoko Kata ya Kisarawe, Kigamboni mkoani Dar es Salaam, ambayo imesajiliwa kwa jina la Rainbow Junior Christian.

Anasema kutokana na jina la Rainbow kuhamia Kisarawe II, TPC imelazimika kuibadilisha shule ya Toangoma jina.
“Tunaona ni mkakati wa wazi wa hawa wamishionari kutoa huduma kwa mrengo wa kibiashara zaidi. Wamelindana na kuwezeshana, halafu wanaumiza watoto wa Tanzania,” anasema.

Mzazi mwenye watoto wawili shuleni hapo ambaye naye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, anasema menejimenti iliyojenga shule mpya iliharibu shule ya awali kwa makusudi, huku uongozi wa TPC ukijua.

“Haiwezekani shule irudishwe TPC Februari, halafu waje waichukue rasmi Oktoba, miezi nane baadaye. Walikaa kimya makusudi wakimwezesha mchungaji wao aliyeshindwa kesi ili ajijenge. Waliacha hadi kufundisha watoto na kila tulipofuatilia, walisema wanashughulikia,” anadai.

Anasema hali haikubadilika na kwamba, mwezi Julai, mwaka huu, walipata fununu kupitia kwa wanafunzi kuwa wamiliki wa shule hiyo, wanajenga shule nyingine.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Awali na Msingi Rainbow Junior Christian, Julieth Nzally, anafafanua madai hayo kwamba, ujenzi wa shule hiyo mpya una baraka zote za serikali na kwamba wamekubaliana na baadhi ya wazazi kuhamisha watoto.

SERIKALI YACHUNGUZA

Akizungumza na Nipashe kuhusiana na sintofahamu hiyo, Kamishna wa Elimu Tanzania, Dk. Lyabwene Mtahabwa,  alisema kilichofanyika shuleni hapo ni kinyume cha utaratibu, kanuni na mwongozo wa shule, unaotaka haki ya mtoto ilindwe katika mazingira yoyote.

Kutokana na hali hiyo, Dk. Mtahabwa amewaelekeza wadhibiti ubora kwenda kukagua shule hiyo ili kubaini chanzo cha kufungwa kwake.

Alisema uamuzi wowote haupaswi kuathiri wanafunzi na badala yake, uongozi huo unapaswa kuhakikisha maslahi ya wanafunzi kusoma yanalindwa.


HUKUMU YA KESI
Katika kesi hiyo, wachungaji hao Jung Hwan Kim na mkewe Sang Ok Nam, raia wa Korea Kusini, walishindwa kesi ambayo walikuwa wanadai fidia ya Sh. bilioni 1.4, walizodai walizitumia kujenga Shule ya Msingi ya Rainbow.

Hukumu hiyo iliyotolewa na Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam na  walidai kuwa walijenga shule hiyo kwa fedha zao na michango kutoka kwa rafiki zao.

“Ninatamka kuwa mali Shule ya Rainbow na mali nyingine zote ni za Kanisa la Presbyterian Tanzania…nawaagiza Jung Hwan Kim na Sang Ok Nam kusalimisha usimamizi wa Shule ya Msingi ya Rainbow na mali zake zote kwa Kanisa la Presbyterian Tanzania,” alisema Jaji John Nkwabi, katika hukumu yake ya Februari 5, mwaka huu.

Katika hukumu hiyo, Jaji Nkwabi alizingatia baadhi ya masuala, ikiwa ni pamoja na iwapo Wamishenari hao wawili walikuwa waanzilishi, wamiliki na wafadhili wa shule ya Rainbow. Alizingatia kama Rainbow ulikuwa mradi wao chini ya mwavuli wa TPC.

Jaji Nkwabi alisema cheti cha usajili wa shule hiyo kinaonesha kuwa mmiliki ni TPC, huku msimamizi wa shule hiyo akiwa ni Jung Hwan Kim.

Pia alisema Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) pamoja na hati ya eneo shule ilipojengwa vipo kwa jina la Tanzania Presbyterian Church.

“Hiyo inathibitisha vya kutosha kuwa mshtakiwa (Kanisa la Presbyterian Tanzania) ndiye mmiliki wa shule. Walalamikaji (Jung Hwan Kim na Sang Ok Nam), wameshindwa kuthibitisha kuwa wanamiliki shule hiyo,” aliamua.

“Kwa vyovyote vile, alisema, ushahidi wa mashahidi wa walalamikaji unaonekana kuwa na chuki dhidi ya mshtakiwa kwa sababu walifukuzwa kazi katika Shule ya Awali na Msingi ya Philadelphia ambayo pia, iko chini ya mshtakiwa (TPC).”

Aidha, alisema ni jambo lisilowezekana ingawa walalamikaji wanaeleza kuwa stakabadhi hizo hazipo katika majina yao bali zipo kwenye jina la shule, wanataka kulipwa fidia na mshtakiwa ya Sh. 1,417,152,600 bila uthibitisho wowote kama walitumia fedha zao.

Alisema sheria hairuhusu fidia hiyo kulipwa kwa kuwa inataka upande wa mlalamikaji kuthibitisha tuhuma ilizowasilishwa mahakamani.