Wajeruhiwa na mafuta petroli yaliyohifadhiwa ndani ya duka

By Moses Ng’wat , Nipashe
Published at 09:44 AM Dec 21 2024
Wajeruhiwa na mafuta petroli  yaliyohifadhiwa ndani ya duka
Picha: Mtandao
Wajeruhiwa na mafuta petroli yaliyohifadhiwa ndani ya duka

WATU wanane wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi iliyoko Mjini Vwawa, baada ya kujeruhiwa katika ajali ya moto baada ya duka la kuhifadhi na kuuza vinywaji vya jumla na rejareja (depo) kuwaka moto.

Inadaiwa kuwa moto huo umesababishwa na mafuta ya petroli yaliyohifadhiwa ndani ya duka hilo.

Ajali hiyo ilitokea juzi katika kijiji cha Ihowa, Kata ya Luanda, wilayani Mbozi, kwenye nyumba ambayo pia hutumika kama duka la kuuza vinywaji vya jumla na rejareja.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ihowa, Spidi Mbembela, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa, majeruhi wengi wa ajali hiyo ni wale waliofika eneo la tukio kwa lengo la uokoaji.

Alisema chanzo cha ajali hiyo kinadaiwa ni baada ya kulipuka kwa dumu la mafuta ya petroli ambalo lilikuwa limehifadhiwa ndani wakati mama mwenye nyumba hiyo, Rose Patrick, akiaanda chakula ndani ya duka hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari, mganga aliyekuwa zamu katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi, Dk. John Mwanyingili, alikiri kupokea majeruhi hao wanane juzi saa 12:00 jioni, ambao wamefanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu.

Dk. Mwamyingili alisema majeruhi hao ni pamoja na Rose mwenyewe na wengine ni Isambi Mwene (34), Maneno Jullius (49), Fadhiri Festo (32), Lewis Patrick (19), Frank Msyan (40) na Matokeo Islam (51).