RC ageuka mbogo kukithiri mauaji, ukatili

By Elizabeth John , Nipashe
Published at 09:45 AM Dec 21 2024

 MKUU wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka.
Picha:Mtandao
MKUU wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka.

MKUU wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, amekuja juu na kuhoji kukithiri kwa matukio ya mauaji, ukatili wanawake na watoto mkoani hapa kama ni matatizo ya afya ya akili au ushetani.

Mtaka alitoa kauli hiyo kwenye kikao na makundi mbalimbali kichofanyika mjini hapa juzi kujadili jinsi ya kukabiliana na matukio hayo katika jamii.

Ni baada ya kueleza kuchukukizwa kwake na kukithiri kwa matukio hayo na kuchafua sifa ya mkoa huo.

Alisema matukio hayo yanaondoa ubinadamu na kufedhehesha utu wa mtu na haki katika jamii, hivyo hayavumiliki na hayapaswi kuendelea kutokea mkoani hapa.

“Kwa kweli ni matukio ambayo binafsi yamenifedhehesha sana, yamenisikitisha sana, tunataka kujenga jamii ipi, huu utamaduni unatoka wapi?” alihoji Mtaka.

“Nadhani serikali tumezungumza hili jambo kijuu juu sio kwenye uzito ambao unafanana na hiki kinachotokea hizi siku za karibuni, mtaona huko mitandaoni matukio kila unaposoma unajiuliza yanafanywa na binadamu kabisa mwenye akili timamu,” alisema.

Mataka alisema tofauti na mikoa mingine nchini kamanda wa polisi anashughulika na matukio ya uhalifu, lakini kwa Njombe mengi yanafanywa ndani ya familia.

“Sasa imekuwa kazi ya Jeshi la Polisi  kuripoti leo kuna kituko hiki, ni matukio ambayo yapo nje ya uwezo wa kusema Polisi wameshindwa kufanya kazi yao,” alisema.

Mtaka alisema jamii na kila mmoja kwenye nafasi yake ya uongozi au mazingira, anapaswa kuzungumza kwa uzito mkubwa.

“Hatuwezi kuwa na mkoa ambao ukiamka unaona mitandaoni mwanamke kakata mwanaume sehemu za siri sasa hapo RPC (Kamanda wa Polisi Mkoa) anahusikaje? Mara kuna mwanaume ameingiza mkono kwenye maumbile ya nyuma ya mwanamke katoa utumbo, sasa hapo polisi anahusikaje,” alisema.

Alisema kama tatizo ni afya ya akili, viongozi wa dini wanapaswa kuhubiri katika nyumba za ibada kuhimiza waumini wao wakapimwe na kupatiwa ushauri wa kisaikolojia.

“Viongozi wa siasa, sasa tuzungumze, tujiseme, tusemane, unasoma mitandao mpaka unashangaa  sisi mkoa tumepata shida gani, “ alisema Mtaka.

Hata hivyo, alisema historia ya mkoa huo, matukio ya visa mara watoto wamefanya hivi mara vile, wakati wengine huoni ushirikina bali unaona ushetani, alisema Mtaka.

 Akitoa takwimu za matukiao hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahmoud Banga, alisema kuanzia mwaka 2021 hadi Desemba mwaka huu, matukio 279 ya mauaji yaliripotiwa katika vituo vya jeshi hilo.

 Kwa mujibu wa Banga, ukatili wa kijinsia kwa ubakaji zaidi ya 820 yaliripotiwa.

Alisema kwa makosa ya ulawiti 91 yaliripotiwa, watoto wadogo kuanzia miaka mitatu hadi 17 ndio  waathirika na kwa watu wazima kuanzia miaka 18 na kuendelea.

Kamanda Banga alisema uchunguzi wao umebaini kuwa wanaolawitiwa ni watoto wadogo kati ya miaka mitatu hadi miaka 17 ndani ya familia na kufanywa siri.

“Kuongezeka kwa matukio hayo ni kutokana na kuzidi kuelimisha jamii na watu wanajitokeza vituo vya polisi kutoa taarifa,” alisema.

Kuhusu mauaji, Banga alisema ni kutokana na imani za kishirikina, migogoro ya ardhi, familia na wivu wa mapenzi.

Mmoja wa wakazi mkoani Njombe, Joram Hongoli, alisema kukithiri kwa  matukio ya ukatili dhidi ya watoto kutokana na wazazi na walezi kujiondoa katika jukumu la malezi na kuwaacha wakizagaa mitaani bila uangalizi.