Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ametoa wito kwa wazalishaji wa taulo za kike kuhakikisha bidhaa hizo zinapatikana kwa gharama nafuu kwa wanafunzi na wanawake wanaoishi vijijini.
Waziri Ulega alitoa kauli hiyo alipokuwa akitembelea banda la Kampuni ya Dowercare Technology, wazalishaji wa taulo za kike, taulo za watoto, na taulo za kujifutia, katika kiwanda chao kilichopo Kibaha.
Waziri alisema baadhi ya wanafunzi na wanawake wa vijijini wanashindwa kumudu gharama za taulo hizo, hivyo ni muhimu kuhakikisha bidhaa hizi zinawafikia kwa bei rafiki. Aliongeza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wawekezaji nchini kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili, ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara.
Afisa Masoko wa Kampuni ya Dowercare Technology, Lucia Msami, aliishukuru serikali kwa ushirikiano mkubwa wanaopata katika shughuli zao za uwekezaji na uzalishaji. Alisema kampuni hiyo tayari imeanza kuchukua hatua za kupunguza gharama za taulo za kike, ambapo wanafunzi wanauziwa taulo hizo kwa Shilingi 1,200.
Lucia alieleza kuwa wanawake wa vijijini pia wananufaika na bidhaa hizo kupitia mtandao wa mawakala wa kampuni hiyo. Kwa mwaka 2023 na 2024, kampuni imefanikiwa kusambaza taulo 20,000 kwa wanafunzi, na inaendelea na juhudi za kuwafikia walengwa katika maeneo mbalimbali.
Aidha, Lucia alisema Dowercare Technology imekuwa ikitoa zawadi za taulo za kike kwa wanawake wanaojifungua katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambapo wanapewa taulo za bure kwa kipindi cha mwaka mmoja. Mpango huo unatarajiwa kupanuliwa hadi hospitali za Temeke na Tumbi, ambapo wanawake wanaojifungua pia hupatiwa elimu ya matumizi bora ya taulo hizo na jinsi ya kuzihifadhi ili kulinda mazingira.
Lucia alitoa wito kwa Watanzania kuunga mkono bidhaa zinazozalishwa nchini, hasa zile zinazotengenezwa na Dowercare Technology, kwani zina gharama nafuu na zinalenga kuboresha maisha ya wananchi wote.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED