TUGHE yawasilisha hoja sita kwa serikali

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 06:18 PM Dec 20 2024
Katibu Mkuu wa TUGHE, Hery Mkunda.
Picha:Mpigapicha Wetu
Katibu Mkuu wa TUGHE, Hery Mkunda.

CHAMA cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) kimetoa hoja sita kwa serikali ikiwamo kuomba ufanyike ukaguzi mahsusi kwa sekta binafsi kutokana na ajira nyingi ni za mikataba jambo ambalo linasababisha wafanyakazi kunyanyasika kwa kukosa uhakika wa ajira zao.

Akisoma risala ya chama hicho  kwenye mkutano mkuu wa TUGHE ulioenda sambamba na maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, Katibu Mkuu wa TUGHE, Hery Mkunda;

Amesema ukaguzi huo utasaidia kubaini ukubwa wa tatizo na kufanya marejeo ya Sheria ili kuboresha eneo la aina ya mikataba ya ajira na adhabu kwa waajiri wanaozuia wafanyakazi kujiunga na vyama vyao.

“TUGHE tunawakilisha wafanyakazi toka katika Taasisi binafsi zinazotoa huduma ya afya. Katika taasisi hizi pamoja na taasisi nyingine binafsi, imekuwapo changamoto kubwa ya muda mrefu ya wafanyakazi kukosa ulinzi wa ajira zao,”amesema.

 Ameeleza kuwa ajira nyingi katika sekta binafsi ni ajira za mikataba ya muda mfupi kuanzia ajira za vibarua, ajira za mwezi mmoja hadi miezi mitatu jambo ambalo linawanyima uhakika wa ajira zao.