VIONGOZI wa kisiasa na serikali mkoani hapa wametakiwa kutafsiri dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2025-2050 kwa manufaa ya wananchi.
Wito huo ulitolewa juzi na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, wakati wa hafla ya uzinduzi wa hamasa ya uandikishwaji katika daftari la mpigakura Wilaya ya Njombe.
Chongolo alisema moja ya kosa ambalo limewahi kufanyika ni kutoitafsiri dira hiyo kutokana na changamoto za Mkoa wa Njombe.
Alisema viongozi hao wanatakiwa kujipanga kutafsiri dira hiyo kwa kuihusisha na namna ambavyo mkoa huo unaweza kunufaika na fursa za kiuchumi kutokana na kuwa lango la kimataifa la biashara kwa kuwa nchi nyingi zilipitisha mizigo hasa Makambako.
“Sasa hivi tuna dira mpya ambayo inaanza mwaka kesho, itaenda kwa miaka 25 tujipange kuitafsiri kwa sura hiyo, Njombe hili ni lango la mikoa mingi, na ni lango la mataifa, hakuna mzigo unaotoka Zambia bila ya kupita hapa,” alisema Chongolo.
Aliwataka viongozi hao kuachana na tabia ya ubinafsi kwa kuwawezesha vijana kupata fursa za kiuchumi ili kukuza kipato chao.
Awali Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama hicho Wilaya ya Njombe, Erick Ngole, aliwataka vijana kuhamasisha wananchi kushiriki katika uboreshaji wa daftari la kudumu la mpigakura ili wapate sifa ya kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED