HUU ni wakati wa usajili wa dirisha dogo, ambalo hufunguliwa kwa lengo la kuzisaidia klabu kusajili wachezaji wa kuongeza nguvu kwenye vikosi vyao.
Walioleta mfumo huu walikuwa na lengo la kuwasaidia viongozi na makocha kurekebisha au kuimarisha vikosi vyao baada ya mechi za mzunguko wa kwanza.
Wakati mwingine timu inakuwa imeshaanza kuwa na majeruhi, au baadhi kushuka viwango, lakini inawezekana usajili wa mwanzo wa msimu haukukidhi matarajio, hivyo ni kipindi cha kuziba mapengo ambayo yalionekana wakati mechi za mzunguko wa kwanza zikiendelea.
Tumeona baadhi ya makocha ambao walijiunga na timu mara baada ya walimu wa mwanzo kutimuliwa wakilalamika kukuta kuna mapungufu makubwa kwenye vikosi vyao.
Hata baadhi ya viongozi nao wameonekana kuzungumzia mapungufu ya vikosi vya wakati michezo ikiendelea.
Mfano, mmiliki wa Fountain Gate, Japhet Makau, amebainisha wazi kuwa kikosi chao pamoja na kwamba kina safu bora ya ushambuliaji, lakini kimeonekana kuwa na matatizo upande wa ulinzi.
Akabainisha kuwa kipindi hiki watafanya kila njia ili kusajili wachezaji ambao watakuja kuimarisha ukuta.
Kocha Mkuu wa KenGold, Omari Kapilima, naye ameilalamikia safu yake ya ulinzi kuwa haipo vizuri, akawa analisubiri dirisha dogo ili kufanya usajili kutatua tatizo hilo.
Makocha kama Juma Mwambusi wa Coastal Union na Juma Mgunda wa Namungo FC nao wameelezea kuwa watafanya usajili ili kufanya maboresho kwenye vikosi vyao, kwani wamevikuta kuna maeneo vina mapungufu.
Hii inaonesha kuwa kuna uhitaji mkubwa wa wachezaji kipindi hiki cha dirisha dogo.
Ingawa mara nyingi inasemekana katika kipindi hiki huwa hakuna wachezaji wazuri sana wanawekwa sokoni na klabu nyingi hazipendi kuuza wachezaji kipindi hiki kwani huwa kwenye ligi na michuano mingine, lakini wale wa kuziba mapungufu machache yaliyopo wanapatikana.
Si kwenye Ligi Kuu ya soka la wanaume tu, hata katika timu ya soka wanawake pia zipo timu zinahitaji kufanya usajili kwa ajili ya kuboresha vikosi vyao.
Mfano, Yanga Princess inaonekana ina shida kwenye upande wa kiungo mshambuliaji na straika wa kupachika mabao, Simba Queens ikiwa na tatizo kubwa la golikipa, pamoja na straika mmoja wa kumsaidia Jentrix Shikangwa, hasa baada ya kuondoka kwa Aisha Mnunka, JKT Queens ikitakiwa kuongeza kiungo mshambuliaji wa kupiga pasi za mwisho na zingine ambazo zinaonekana zina mapungufu makubwa zaidi ya hizi nilizozibainisha.
Ni wakati wa viongozi wa klabu kuwaunga mkono makocha na kuwaletea kile ambacho wanakihitaji na si kile ambacho wao wanapenda kukileta.
Kuna baadhi ya viongozi husajili wachezaji kwa matakwa na mapenzi yao binafsi, kocha anataka beki wa kati, lakini wanasajili mastraika kwa sababu tu ni mchezaji mwenye jina ili apate sifa.
Matokeo yake ligi inaisha timu haipati matokeo mazuri anayefukuzwa ni kocha kwa kuonekana hajafanya vizuri, kumbe tatizo lipo kwa viongozi ambao wameshindwa kumletea kocha wachezaji anaohitaji.
Kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili ni wakati wa viongozi kuwasikiliza makocha wanataka nini, kuwatekelezea wanachohitaji, ili kuwahukumu kwa haki mwishoni mwa msimu.
Binafsi, ningependa hukumu ya haki mwishoni mwa msimu, kama viongozi wamevurunda kwenye usajili basi wajitathimini wenyewe na kama kocha ameletewa kila kitu na ameshindwa, basi awajibishwe.
Nisingependa kuona viongozi wakiwa na visingizio vingi mwishoni mwa msimu na kumalizia kwa kuwabebesha lawama makosa, au makocha kuwanyoshea vidole viongozi ambao wachezaji walionao na wakashindwa kuwapa walichokihitaji.
Timu zisajili vizuri, hatutaki visingizio mwishoni mwa msimu.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED