Vijana sikukuu kuweni makini

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 11:12 AM Dec 25 2024
Vijana sikukuu   kuweni makini.
Picha:Mtandao
Vijana sikukuu kuweni makini.

HERI ya Noeli vijana. Imekuwa ni kawaida kwa baadhi yenu hasa wakazi wa mijini kuchangishana fedha na kukodi magari kwenda ufukweni kusherehekea sikukuu.

Mkiwa huko mnaogelea na kufanya mambo mengine ya burudani pamoja na  matendo yanayokiuka maadili.
 
 Katika safari zenu za kwenda ‘beach’ au ufukweni, mwendo ambao dereva huendesha, si wa usalama bila kujali kuwa wapo wengine wanaoning'inia madirishani na wengine milangoni.
 
 Mkiwa katika mazingira hayo, mnajisahau mnashangilia na kupiga kelele kumhimiza dereva kuongeza mwendo.

Ili kukoleza mukari wapo wanaogonga gari na kupuliza mavuvuzela kwa raha zao kana kwamba wanachokifanya ni sahihi.
 
 Vijana hao wanapokuwa katika safari hiyo wana vinywaji vikali ndani ya gari, wengine wameshakunywa  kitendo kinachoashiria kuwa wanakwenda kulewa na licha ya kwamba wengine  walianza kulewa kabla ya safari.
 
 Leo ni Sikukuu ya Krismasi, ninaomba niwakumbushe vijana wenye mtindo huo kuwa ni vyema washerehekee kwa umakini, wasiruhusu kujiweka katika mazingira hatarishi kama ambavyo wamezoea kufanya.
 
 Si vibaya kukodi gari kwenda beach, lakini ni vibaya kukodi gari na kumtaka dereva aendeshe mwendo ambao si salama kwao na pia si salama kwenda huko na kufanya vitendo visivyofaa ukiwamo vya ngono.
 
 Ninaamini kwamba mtu anapozidiwa na pombe, anaweza kufanya vitendo visivyofaa, hivyo, hata madereva wanaokodishwa kwenda kusherehekea sikukuu wakilewa, ni hatari zaidi kwa hao waliokodisha gari.
 
 Watahoji kwa nini sababu ni kwamba umakini wawapo barabarani unapotea na kujikuta wakisababisha ajali ambazo wakati mwingine zingeweza kuzuilika iwapo wangekuwa makini kwa kuepuka kunywa vilezi na kuendesha magari.
 
 Vilevile madereva wa bodaboda nao hawako nyuma. Kila siku baadhi yao hukesha wakilewa kwa mtindo ambao wanauitwa 'kutoa loki'. Hao nao wakati wa sikukuu huwa wanalewa pombe zaidi hasa ‘viroba.’
 
 Sio kwamba wanalewa na kurudi nyumbani, bali huingia barabarani kubeba abiria, tena wakati mwingine  zaidi ya mmoja (mishkaki) bila kujali kwamba wanaiweza na kujikuta wakiwabwaga.
 
 Kitendo hicho kinaweza kusababisha wenyewe na abiria wao kupoteza maisha au kupata ulemavu wa kudumu na hivyo kujikuta wakiwa tegemezi kwa familia au kwa ndugu na jamaa.
 
 Ninadhani kwa wakati huu wa sikukuu ipo haja kwa vyombo vya dora kuongeza mikakati ya kukabiliana na watu wa aina hiyo ili kuokoa maisha yao badala ya kuwaacha wakisherehekea wanavyotaka.
 
 Biashara ya bodaboda inagharimu maisha ya watu kutokana na uzembe wa baadhi ya madereva wake kwa kutozingatia maelekezo wanayopewa ili waweze kuwa salama wakati wote wanapoendesha vyombo hivyo.
 
 Wengi wa madereva wa bodaboda ni vijana ambao wanategemewa kuwa taifa la sasa na la kesho, lakini inasikitisha kuona baadhi yao wakijihusisha na ulevi huku wakiendesha vyombo vya moto.
 
 Sheria ziko wazi kwamba mtu hawezi kuendesha chombo cha moto akiwa amelewa, hiyo ni kwa ajili ya usalama wake na wale aliowabeba, lakini ajabu ni kwamba vijana waVijana sikukuu   kuweni makini.hilo.
 
 Pamoja na katazo hilo, imekuwa ni kawaida kwao kulewa siku zote. Kwa hali kama hiyo, ni wazi kwamba wakati wa sikukuu wanaweza kujiachia zaidi bila kujali usalama wao na hata wa abiria wao.
 
 Mazingira hayo ndio yanayonisukuma kuwashauri wawe makini kwamba kuna maisha baada ya sikukuu, hivyo, uhai ni muhimu kuliko sikukuu ambazo huzichukuliwa kuwa ni za kulewa kupita kiasi.
 
 Niwatakie sikukuu njema yenye amani na utulivu itakayoisha bila kuwapo ajali za kizembe zinazotokana na ulevi wa kupindukia ambao unagharimu maisha ya watu na kuangamiza nguvu kazi ya taifa.