JESHI la Polisi mkoani Lindi linamshikilia mkazi wa kijiji cha Mtumbya, kata na Halmashauri ya Mtama, Hassani Omari (30) kwa tuhuma za mauaji na wizi wa mali.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) John Imori alitoa taarifa hiyo jana alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali.
Alisema mtuhumiwa huyo anadaiwa kufanya tukio la mauaji na wizi Desemba 10 mwaka huu, saa mbili usiku baada ya kumkodi dereva pikipiki Azizi Omari (28) kwa lengo la kumpeleka sehemu alikotaka.
Kamanda Imori alisema kuwa tangu bodaboda huyo akodiwe na mtuhumiwa, hakuonekana tena katika maeneo alikokuwa anafanyia biashara yake.
Alisimulia kuwa Desemba 22, mwaka huu, saa 11 jioni, mwili wa kijana huyo uliokotwa porini katika kijiji cha Mtumbya, jambo lililothibitisha kuwa aliuawa.
"Huyu bodaboda alikodiwa na mtuhumiwa ili ampeleke safari yake, lakini kuanzia hapo hakurejea hadi mwili wake ulipokutwa porini," alisema Kamanda Imori.
Alisema mtuhumiwa alikamatwa katika kijiji cha Mkunya, wilayani Newala, mkoani Mtwara akiwa anaendesha pikipiki ya marehemu yenye namba za usajili MC 559 EAL.
Kamanda Imori alisema mtuhumiwa amesharejeshwa mkoani Lindi na atafikishwa mahakamani muda wowote kuanzia ili kujibu mashtaka yanayomkabili baada ya upelelezi kukamilika.
Kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni za Adhabu, SURA 16, ikiwa mtuhumiwa huyo akipatikana na hatia mahakamani, adhabu ya kosa la kuua kwa kukusudia ni kunyongwa hadi kufa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED