Rombo Marathon yafana, ikifungua milango

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 12:04 PM Dec 25 2024
Rombo Marathon yapata mafanikio makubwa, ikifungua milango.
Picha:Mtandao
Rombo Marathon yapata mafanikio makubwa, ikifungua milango.

MSIMU wa tatu wa mbio hisani za Rombo Marathon 2024, umefanyika kwa mafanikio makubwa, huku Rais mstaafu Dk. Jakaya Kikwete, akifungua milango kwa wanariadha wa Tanzania kujifua katika eneo lenye miinuko, msitu wa asili, na ile inayomilikiwa na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) ya Rongai Forest.

Kikwete, alishiriki Desemba 23 mwaka huu Rombo Marathon na maelfu ya wazawa wa Rombo, wakazi wa mikoa jirani na wenyeji wa Kilimanjaro waishio mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma, Mbeya, Tanga na Zanzibar.

Mbali na mbio hizo, pia alichagiza shamrashamra za wazawa na wageni mbalimbali wa kitaifa ambao ni maarufu, akiwamo Mshauri wa Rais Samia Suluhu Hassan katika masuala ya afya na tiba, Prof. Mohamed Janabi.

Prof. Janabi na watu wengine maarufu, walifurahia mbio hizo baada ya kufika Rombo na kukutana na tamasha la nyama choma maarufu Ndafu Festival, huku amewataka Watanzania kuwa na utamaduni wa kushiriki katika michezo ili kijenga afya. 

Mwasisi na muandaaji wa Rombo Marathon, Prof. Adolf Mkenda, ambaye pia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, amesema mbio hizo zimewahusisha zaidi ya wakimbiaji 1,200. 

Prof. Mkenda, amesema licha ya kuwapo wakimbiaji wengi,  pia zimewavutia watu mbalimbali 5,000 walioingia mkoani Kilimanjaro ‘kuhiji’ sikukuu za mwisho wa mwaka za Krismasi na mwaka mpya. 

Vilevile, Prof. Mkenda, ambaye ni Mbunge wa Rombo, alidokeza kuwa kiasi cha fedha kilichopatikana kitasaidia kuchangia mradi wa upanuzi wa Hospitali Teule ya Huruma, inayoendelea na mchakato wa kutaka kupandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Rufani. 

Baada ya mbio hizo, Prof. Janabi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), amewapa somo wakazi wa Rombo, kunywa maji, akieleza kuwa mandhari ya maeneo hayo yaliyoko uwanda wa juu wa Mlima Kilimanjaro, husababisha damu kuwa nzito.