MWENYEKITI mstaafu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amesema atafanya maombi kwa Mungu kupata upande sahihi wa kuunga mkono katika mvutano wa kumpata mwenyekiti wa chama hicho.
Amesema muda si mrefu ataonesha ni upande gani anaounga mkono kati ya Mwenyekiti wa sasa wa chama hicho, Freeman Mbowe na Makamu wake, Tundu Lissu.
"Kwa sasa sina timu, pengine siku za usoni ninaweza kujali zaidi juu ya mwelekeo wangu kwa nani ninapenda awe kiongozi mkuu kwenye chama chetu.
"Kwa sasa ninatazama, ninafikiria na kusali, kwa sababu hii position (nafasi) wanayoomba ina umuhimu hata kwangu pia kama mwana-CHADEMA," alisema Lema.
Mbowe na Lissu wanagombea nafasi moja ya uenyekiti wa chama hicho taifa na tangu watangaze nia, kumekuwa na mvutano mkubwa mitandaoni kutoka kwa makada na wafuasi wa chama hicho wanaoonekana kugawanyika makundi mawili ya wanaomtaka Mbowe aendelee na wanaomtaka Lissu apokee kijiti hicho.
Akizungumza na Nipashe jana, Lema ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu wa chama hicho alisema kuwa amekuwa mtazamaji na anafikiria kuanza kusali kabla ya kuonesha upande anaounga mkono kati ya vigogo hao wawili.
Lema alisema kuwa kikubwa anachoomba hivi sasa kwenye chama chake ni utulivu kuelekea uchaguzi huo wa ndani ya chama.
"Ninachoomba kwa sasa ni utulivu ndani ya chama, ila hata kama kuna mgombea nitamuunga mkono na kwa sababu atakuwa ni mwana-CHADEMA, sidhani kama litakuwa jambo baya," alisema.
Lema aliyewahi kuwa Mbunge wa Arusha Mjini, alitoa angalizo kwa wanachama na wafuasi wa CHADEMA kwamba katika kipindi hiki cha uchaguzi ndani ya chama, kuna haja ya kuwa makini katika kutoa majibu yanayotokana na hisia za wanachama wanaounga mkono upande wowote wa wagombea.
Vilevile, mstaafu huyo pia alitoa angalizo kwa wanaonyukana kupitia mitandao ya kijamii, akiwataka kuweka mbele maslahi ya chama chao hususani katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwakani.
"Tumetoa maazimio kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka kesho, kwamba ‘no reforms no election’ (hakuna mabadiliko hakuna uchaguzi). Tunatakiwa tuweke nguvu yetu huko, lakini endapo haya yataendelea si tu ni hatari kwa chama chetu, bali pia hata kwa nchi yetu kwa maana chama hiki ndicho kinapigania Katiba mpya na mifumo bora ya uchaguzi ambalo ndilo la msingi kuliko jambo lolote," Lema alionya.
Pia aliwataka wagombea kutumia lugha ya staha na kutambua kwamba chama hicho ni cha wanachama wote.
"Wagombea watambue kwamba hawagombei dhidi ya mashetani, wanagombania nafasi dhidi ya wanachama wote, siasa za heshima si tu zinakijenga chama bali zinakifundisha chama tawala juu ya demokrasia tunayoishi...
"Minyukano, matusi na dhihaka kwenye mitandao itaonesha demokrasia tunayoihubiri tunashindwa kuiweka kwenye vitendo," Lema alionya zaidi.
Alisisitiza hisia na maoni ya wananchi juu ya kile kinachoendelea ndani ya chama hicho vinahitaji kujibiwa kwa tahadhari.
Lema pia alitoa tahadhari dhidi ya matumizi ya rushwa katika uchaguzi huo na kusisitiza yakemewe kwa vitendo.
Lema alisema: "Tunataka matumizi ya rushwa na fedha yakemewe kwa vitendo kuelekea katika uchaguzi wa ndani ya chama chetu, maana tunaposema rushwa ni adui wa haki, hatumaanishi chama tawala pekee, bali tunahusisha vyama vyote vya siasa kwa sababu ukipita kwa rushwa huwezi kuikemea."
Kumekuwa na mnyukano mkali katika mitandao ya kijamii miongoni mwa wafuasi wa Mbowe na Lissu baada ya viongozi hao kuingia katika kinyang'anyiro cha nafasi ya Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa.
Mara kwa mara Mbowe amenukuliwa na vyombo vya habari, likiwamo gazeti Nipashe, akiwataka wanachama na wafuasi wa CHADEMA kutoingia katika mtego wa wabaya wao kisiasa -- kutumia uchaguzi wa ndani kuharibu taswira ya chama hicho.
Lissu, kwa upande wake, amekuwa akijibu tuhuma mbalimbali zinazoelekezwa kwake na baadhi ya viongozi wa CHADEMA wanaoonekana kumuunga mkono Mbowe katika uchaguzi huo, baadhi akiwatuhumu waziwazi kutumiwa na baadhi ya viongozi wa serikali kuharibu ajenda za msingi za CHADEMA.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED