Mwinyi ajivunia barabara mpya kupunguza msongamano, ajali

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 08:47 AM Dec 25 2024
Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Picha:Mtandao
Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka wananchi, kudumisha amani umoja na mshikamano ili kupata maendeleo.

Alitoa rai hiyo jana wakati akizungumza na wananchi katika uzinduzi wa barabara ya Uwanja wa Ndege - Mnazimmoja yenye urefu wa kilomita 6.5 iliyogharimu zaidi ya dola milioni tano.

Alisema ufunguzi wa barabara hiyo ni sehemu ya utekelezaji mradi wa ujenzi wa kilomita 100.9 za barabara za mjini ambazo zilikuwa katika hali mbaya na kujenga barabara za juu ili kupunguza msongamano.

Alisema lazima wahakikishe usafiri unakuwa mzuri katika mji wa Zanzibar kwa kuwa barabara za kisiwa hicho ni finyu na kuwafidia wananchi huwa ni gharama kubwa na ndio maana wameamua kujenga barabara zenye njia mbili.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa baada ya kukamilika kwa ujenzi huo, hakuna nyumba zitakazoingiliwa na maji baada ya kujengewa miundombinu mingine ikiwamo mitaro pembezoni mwa barabara.

Alizungumzia pia matunzo ya barabara hizo, akiwataka madereva kuacha kuegesha gari katika njia za kupita watu kwa miguu.

Alisema kumeanza tabia za ovyo kuweka kifusi na kugeuza maegesho katika njia za watu kupita kwa miguu pembezoni mwa barabara na kutaka mfuko wa barabara kuhakikisha barabara hizo zinakuwa safi muda wote.

Dk. Mwinyi alisema barabara za juu anazojenga zinalenga kutengeneza mazingira mazuri ya barabara na kuwataka wananchi kuacha kujenga pembezoni mwa hifadhi za barabara.

Alisema wanapotaka kujenga barabara, gharama za fidia zinakuwa kubwa kuliko gharama ya ujenzi wa barabara, hivyo watu waache kujenga kwenye hifadhi za barabara na hifadhi hizo kutunzwa.

"Lazima mji uwe safi, hivyo tutafanya programu maalumu kuhakikisha barabara mpya zote zinakuwa na taa ili ziendane na mazingira," alisema.

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk. Khalid Salum Muhammed alisema wameshakamilisha ujenzi wa barabara za kilomita 86, zikiwamo barabara za ndani.

Alisema ujenzi wa barabara zingine unaendelea vizuri na utakamilika kwa wakati (Novemba mwakani). Alisema mafanikio hayo yanatokana na miomgozo na maono ya Rais Dk. Mwinyi anayotoa kwa wizara hiyo.

Alisema wakati barabara hiyo inajengwa kulikuwa na maneno mengi ya kejeli, kwamba barabara haihitaji kujengwa upya ilhali ilijengwa miaka ya 70 na haikuwa inakidhi viwango vya kisasa.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Habiba Hassan Omar, alisema barabara hiyo ni miongoni mwa barabara zenye urefu wa kilomita 100.9 zinazojengwa kisiwani.

Mkuu wa Mkoa Idrisa Kitwana Mustafa alisema barabara hiyo itapunguza ajali na vifo vitokanavyo na ajali za barabarani kisiwani Zanzibar.