Kumbe inawezekana kupata Taifa Stars bora bila kupunguza wageni

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 12:26 PM Jan 06 2025
Taifa Stars.
Picha:Mtandao
Taifa Stars.

MECHI ya ufunguzi wa Kombe la Mapinduzi kati ya Timu ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes, iliyochezwa Ijumaa kwenye Uwanja wa Gombani, Zanzibar, imetuonesha kuwa inawezekana kabisa kuunda kikosi cha Taifa Stars bila kutengeza kanuni ya kupunguza wachezaji wa kigeni kwenye ligi yetu.

Ni mechi kali, iliyokuwa ya ufundi ambayo ilimalizika kwa Zanzibar Heroes kushinda bao 1-0, lililowekwa wavuni na, Feisal Salum maarufu kama 'Fei Toto.'

Achilia mbali matokeo ya mechi, wengi walioishuhudia walishangazwa na vipaji vya wachezaji wa Kitanzania kwa pande zote mbili, Bara na Visiwani.

Wachezaji wengi wametoka kwenye klabu za madaraja ya kati, na hakuna mchezaji yeyote aliyetoka Simba wala Yanga.

Waliocheza mechi ile waliwaonesha mashabiki kuwa mchezaji wa timu ya taifa, hapatikani kwa kurahisishiwa kazi kwa kuwabana wachezaji wa kigeni ili yeye aonekane.

Badala yake anatakiwa kuwekewa mazingira ya kushindana na hao hao wageni wenye uwezo ili aweze kupambana na kupata namba.

Kuna dhana imejengwa kuwa wachezaji wengi wa kigeni wanazuia wa Kitanzania kuonekana. Lakini ukiitazama sana dhana hii imejengwa sana kwenye Klabu za Simba na Yanga na kidogo Azam kwani ndizo timu zinazosajili wachezaji 12 wa kigeni.

Wanasema wageni wapunguzwe, pamoja na kwamba wanaongea kwa jumla, lakini lengo lao kubwa ni timu hizo tu. Kwa sababu kuna timu ya JKT Tanzania, Mashujaa, Prisons zote hizo hazina wachezaji wa kigeni, na zingine ambazo zinasajili wachezaji wa kigeni pungufu ya hao.

Pamoja na hayo, bado kuna kelele kutoka kwa baadhi ya mashabiki kuwa ni wengi sana. Wanachotaka ni kwamba Simba, Yanga na Azam ziwe na wachezaji wengi wa kizawa wawe wanapata namba kwa ajili ya kuitwa timu ya taifa.

Ni kama vile ni lazima mchezaji mzawa acheze au apitie Simba, Yanga ama Azam ili aitwe timu ya taifa.

Ukweli ni kwamba hakuna kanuni hiyo, badala yake kikosi cha Stars kinaundwa na wachezaji wa Kitanzania wanaocheza ligi ya ndani na nje ya nchi ambao wapo kwenye viwango bora kwa wakati huo wanaochaguliwa.

Hata kama hakutoka mchezaji wa Simba au Yanga kwenye kikosi cha Stars, bado haiondoi kuwa ni timu ya taifa. Ndiyo maana tunaona nchi za Afrika Magharibi kama Senegal, Nigeria, Ghana, wanaweza kuita kikosi kikawa na wachezaji wote wanaocheza soka la kulipwa barani Ulaya.

Nadhani na sisi taratibu tunaanza kuondoka huko japo bado watakuwapo wahafidhina ambao hivi majuzi walitaka kanuni ya kuwa na makipa wa ndani tu kwenye Ligi Kuu, jambo ambalo lilipingwa na Rais wa Shirikisho wa Mpira wa Miguu nchini (TFF), Wallace Karia, akisema hawezi kuzipangia timu wawe na makipa wa aina gani, akisema kipa yeyote Mtanzania anatakiwa ashindane ili apate namba kwenye kikosi na si kuwekewa kanuni.

Kwa vikosi vya Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes nilivyoviona, kunaweza kutengenezwa kikosi cha Taifa Stars bora kabisa ambacho kitafanya vema kwenye michuano ya CHAN, kama kitaongezwa na wachezaji wachache tu wazoefu kutoka Simba na Yanga.

Tanzania inaweza pia kuwa na kikosi bora zaidi kuelekea AFCON 2025 na 2027, kama wataongezwa pia wachezaji wanaocheza soka nje ya nchi ambao kwa sasa si haba.

Tuanze kuondokana na dhana kuwa wachezaji bora wenye uwezo wa kucheza Stars ni lazima watoke Simba au Yanga kwani tumeona hata timu za mikoani zinatoa wachezaji wazuri. Hata Zanzibar nako kuna wachezaji wenye vipaji vya hali ya juu, tuziache Simba na Yanga na malengo yao, kwa kuwa si vitalu vya kutengeneza wachezaji wa Stars.