Upimaji maradhi ya moyo sehemu za kazi ni mwafaka, uungwe mkono

Nipashe
Published at 06:57 AM Jan 09 2025
Upimaji maradhi ya moyo sehemu za kazi ni mwafaka, uungwe mkono.
Picha:Mtandao
Upimaji maradhi ya moyo sehemu za kazi ni mwafaka, uungwe mkono.

MARADHI yasiyo ya kuambukiza yamekuwa yakiongezeka nchini mwaka hadi mwaka, hivyo kusababisha nguvu kazi ya taifa kudhoofika na hata kupoteza maisha. Maradhi hayo ni pamoja na magonjwa ya moyo, figo, shinikizo la juu la damu na kusukari.

Kwa  mujibu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), magonjwa hayo  yamekuwa yakitumia mabilioni ya shilingi kwa ajili ya matibabu, hivyo kutishia ustawi wa mfuko huo. 

Katika hospitali kubwa nchini, ikiwamo Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), kumekuwa na taarifa kwamba wagonjwa wengi wanakwenda kupata huduma ya tiba wakiwa katika hatua za mwisho. Hali hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa vifo vviitokanavyo na maradhi hayo. Licha ya vifo hivyo, pia wako watu ambao wamekuwa wakipata matatizo ya kuona na kukatwa baadhi ya viungo vyao kutokana na maradhi ya kisukari.   

Sababu kubwa inayochangia ongezeko la maradhio hayo ni watu wengi kutokuwa na utamaduni wa kupima afya mara kwa mara. Watu wengi huenda hospitalini kwa ajili ya uchunguzi na tiba baada ya afya zao kudhoofu na kukosa nguvu za kuzalisha mali. 

Chanzo kikubwa cha maradhi hayo ni mfumo wa maisha uliosababishwa na watu kula vyakula bila mpangilio hasa vile vya kusindikwa, kula wanga mwingi na nyama nyekundu kwa kiasi kikubwa na kutokufanya mazoezi. 

Kwa wale wanaofanya kazi ofisini, wakiwamo walio katika nafasi za uongozi, wamekuwa wakikaa ofisini muda wote na wanapomaliza kazi huingia kwenye magari kurejea nyumbani. Wanapofika nyumbani wanakaa kuangalia runinga, kula kisha kulala, hivyo kuwa na uwezekano mkubwa wa kukumbwa na maradhi hayo. 

Kutokana na kuwapo ongezeko la maradhi hayo, JKCI imeanzisha huduma ya kuwapima afya ya moyo wafanyakazi wanapokuwa ofisini ikiwa moja ya njia za kukabiliana na tatizo hilo. Uamuzi wa kuanzisha mpango huo umetokana na kubainika kuwa kuwa baadhi ya watu wanashindwa kwenda kupima afya zao kwa kutingwa na majukumu yao ya kila siku.

Taarifa iliyotolewa na kitengo cha masoko cha taasisi hiyo juzi ilisema imebainika kuwa wanafanya mazoezi bila kujua afya zao na wengine wanapata msongo wa mawazo wakiwa kazini, wengine wanaanguka na kupata matatizo mbalimbali kama kiharusi, hivyo mpango huo umeanzishwa kujaribu kunusuru tatizo hilo. 

Iwapo watu watakaofikiwa na huduma hiyo watabainika kuwa na tatizo, taasisi hiyo imesema wataanzishiwa matibabu mapema kabla ya kuwa katika hali mbaya. Kama ilivyoeleza katika taarifa yake, programu hiyo itasaidia kupunguza gharama za matibabu kwa watu ambao wanagundua matatizo yao ya afya zao hali ikiwa mbaya kwa kuwa utambuzi wa tatizo katika hatua za awali hupunguza gharama za matibabu. 

Kwa ujumla, mpango huo ni mwafaka na umebuniwa katika muda ambao huduma za matibabu zikiwamo upimaji wa afya zikiwa zinahitajika kwa kiwango kikubwa. Kwa mantiki hiyo, mpango huo unapaswa kuungwa mkono na wadau mbalimbali wakiwamo waajiri kwa kupanga muda maalumu kwa wafanyakazi wao kupatiwa huduma za upimaji. 

 Kwa kuwa mpango huo una lengo la kuhakikisha rasilimali watu nchini inakuwa na afya bora, wadau pia hawana budi kujitokeza kuunga mkono kupitia udhamini wa aina mbalimbali. Mpango huo una gharama kubwa zikiwamo usafiri na vifaa, hivyo taasisi zinaweza kutoa msaada kwa watumishi wa JKCI kuwafikia walengwa na kufanikisha jambo hilo kwa ufanisi mkubwa.