Samia akerwa matokeo mabaya mitihani

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 10:34 AM Jan 09 2025
Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Misufini iliyoko Bumbwini, Zanzibar baada ya kuifunguza jana, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
PICHA: IKULU
Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Misufini iliyoko Bumbwini, Zanzibar baada ya kuifunguza jana, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

RAIS Samia Suluhu Hassan, ameeleza kukerwa na matokeo mabaya ya elimu kwa wanafunzi wa shule za Zanzibar kwa madaraja ya sifuri na la nne na kusema hataki tena kuona hali hiyo ikiendelea.

Akizungumza jana wakati wa ufunguzi wa Shule ya Sekondari Bumbwini Misufuni, Mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwa sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi, Rais Samia alisema hakuna sababu ya Zanzibar kuwa na matokeo mabaya kwa sababu serikali inajitahidi kuboresha miundombinu ya elimu kwa kujenga shule za kisasa.

Alisema miongoni mwa malengo ya Mapinduzi ni kuwaletea maendeleo wananchi na waasisi wa Mapinduzi hayo waliweka misingi mizuri na waliendana na malengo ya dini kwa kuhakikisha jambo la kwanza ni elimu na kutoa elimu bure.

Rais Samia alisema alianza kusoma darasa la kwanza mwaka 1965 baada ya Mapinduzi na alisoma katika Shule ya Msingi Kitogani iliyojengwa kwa makuti, maarufu ikiitwa Mabanda ya Mbuzi.

Baada ya Mapinduzi, alisema viongozi awamu kwa awamu waliboresha misingi ya elimu kwa kujenga shule nzuri.

Alisema zamani Zanzibar ilikuwa nyuma kiufaulu kwa sababu hakukuwa na maabara za kisasa, hivyo kwa sasa lazima wanafunzi wasome kwa bidii na kufaulu.

Kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar, alisema kulikuwa na shule 92 zikiwamo sekondari tano na chekechea moja pekee lakini hivi sasa kuna shule 1,308.

"Malengo ya Mapinduzi ni kustawisha hali za wananchi wake, zikiwamo kielimu na kiafya," alisema.

 Rais Samia alisema maono ya serikali ni kuzalisha wataalamu wenye ujuzi ili kusaidia taifa lao na kubainisha kuwa kazi nzuri haijafanyika kuzalisha wataalamu katika sekta ya utalii na pengine kulichangiwa na utamaduni wa kuonekana kuwa kazi hizo hazina staha ndiyo maana Wazanzibari ni wachache katika ajira kwenye eneo hilo.

Aliwataka wazazi kuhakikisha watoto wanasoma kwa bidii ingawa serikali inabeba msaada wa kutoa elimu bure, hivyo panapohitajika wazazi kutosita kusaidia.

Pia aliwataka makandarasi na washauri elekezi wa majengo kufanya kazi kwa uadilifu ili majengo yanayoendelea kujengwa yawe bora na ya kiwango ili yadumu kwa muda mrefu.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Muhammed Mussa, alisema serikali zote mbili zimewekeza kwa kiasi kikubwa kuboresha miundombinu, maslahi ya walimu na vitendea kazi katika sekta ya elimu.

Alisema hali hiyo imesaidia kupata mafanikio katika sekta hiyo ikiwamo kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya taifa.

Waziri Lela alisema hayo ni matunda ya Mapinduzi na wanafunzi wanasoma katika mazingira bora na ni dhamira ya serikali kutoa elimu bora inayokwenda na wakati ulimwenguni.

Alisema katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Dk. Mwinyi, Wizara ya Elimu imejenga shule 35 za ghorofa na 28 ziko katika hatua za ujenzi, ukarabati wa shule zote chakavu, kukamilisha ujenzi wa madarasa yaliyoanzishwa na wananchi ili wanafunzi kusoma katika mazingira rafiki.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Abdallah Khamis Said, alisema ujenzi wa shule hiyo ni juhudi na serikali kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani na ulianza Septemba, 2023 na kukamilika mwishoni wa mwaka 2024.

Alisema thamani ya ujenzi huo ni Sh. bilioni 6.1 na ni ya ghorofa tatu na ina madarasa 40, maktaba, maabara, mabweni ya wanafunzi, nyumba za walimu na ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,841 kwa wakati mmoja.

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Zahro Mattar, alisema kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar, mkoa huo ulikuwa na shule zisizozidi tatu lakini hivi sasa una shule 152 kwa ngazi mbalimbali kuanzia maandalizi, msingi na sekondari.