FEDHA za Mfuko wa Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara, ambazo ni Sh.milioni 75.7 zimetumika kununua vifaa vya ujenzi wa shule mbalimbali jimboni humo ikiwa ni sehemu ya kuboresha elimu.
Hayo yamesemwa na mwenyekiti wa mfuko huo, ambaye pia ni Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo alipokuwa akizungumza na gzeti hili kuhusu mkakati wa kuinua elimu jimboni mwake.
Mbunge huyo amesema wiki iliyopita, Kamati ya Mfuko wa Jimbo ilitembelea ofisi za halmashauri ya wilaya ya Musoma zilizopo Kijiji cha Suguti ili kuainisha vifaa vya ujenzi vitakavyonunuliwa na fedha za mfuko wa jimbo kwa ajili ya shule mbalimbali.
"Fedha za Mfuko wa Jimbo ni Sh. milioni 75.7, vifaa vya ujenzi vitakavyonunuliwa ni saruji mifuko 1,970, mabati ya rangi 322 na nondo 430 za milimita nane," Prof. Muhongo amesema.
Prof. Muhongo amezitaja baadhi ya sekondari zilizogawiwa vifaa vya ujenzi kuwa ni Muhoji, Nyasaungu, Rukuba na zile zinazokamilisha ujenzi wa maabara za masomo ya sayansi.
"Sekondari zilizokamilisha za masomo ya sayansi ni Mtiro, Makojo, Nyambono, Bwai, Mkirira, Etaro na zinazoanza ujenzi wa maabara za masomo hayo ambazo ni Bukwaya na Nyanja," amesema.
Amezitaja nyingine zilizofaidika na fedha za mfuko wa jimbo kuwa ni i za Chitare, Mwigombe, Mmahare, Musanja, Kataryo na Nyabakangara ambazo wananchi wako kwenye harakati wa ujenzi.
"Musoma Vijijini tuna vijiji 68 na sekondari 26 za serikali, huku mbili zikiwa za binafsi, mkakati wa kujenga sekondari kila kijiji, hivyo tunafanya kila njia kufanikisha hilo," amesema.
Ofisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Majidu Karugendo alisema mkakati huo wa kuwekeza kwenye elimu ndio ambao serikali imekuwa ikiupigia debe kila uchao.
"Kipaumbele chetu katika maendeleo ni elimu, ndio maana tunaendelea na mkakati wa ujenzi wa sekondari kwa nguvu za wananchi kwa kushirikiana na serikali. Tumshukuru mbunge Profesa Muhongo kwa kuunga mkono juhudi hizo," amesema Karugendo.
Amefafanua kuwa huenda mwaka huu baadhi ya sekondari zikafunguliwa ili kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza na nyingine kupandisha na kuwa na kidato cha tano na sita kwa mchepuo wa masomo ya sayansi.
Kuna sekondari mbalimbali za vijiji zinaendelea kujengwa zikiwamo za Rukuba Island, Nyasaungu, Muhoji, Butata, Nyamrandirira Technical, David Massamba Memorial, lakini pia kiuna sita za vijiji vya Chitare, Kataryo, Kiriba, Mmahare, Musanja na Nyambono ambavyo vimepata vibali vya kuanza kujenga sekondari," amesema.
Elimu huyo amesema kasi ujenzi wa sekondari ambayo wananchi wanaendelea nayo kwa kushirikiana na serikali, miaka michache ijayo kila kijiji kitakuwa na sekondari yake na kuwapunguzia wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata elimu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED