Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) unaendelea kufanikisha malengo yake ya kufikisha elimu ya hifadhi ya jamii kwa makundi mbalimbali ya wananchi.
Hivi karibuni, wajasiriamali wa Soko la Tegeta Nyuki, jijini Dar es Salaam, wamehamasika kujiwekea akiba baada ya kupata elimu kutoka NSSF kuhusu umuhimu wa hifadhi ya jamii na mafao yanayotolewa.
Kupitia Meneja wa Sekta Isiyo Rasmi, Rehema Chuma, NSSF imeweka kambi ya siku nne katika masoko ya Tegeta Nyuki na Kawe. Lengo la kambi hiyo ni kutoa elimu ya hifadhi ya jamii, kuandikisha wanachama wapya, na kuhamasisha uchangiaji. Kambi hiyo imepokelewa vyema, na hamasa ya wajasiriamali kujiunga imekuwa kubwa.
Akizungumza jana Januari 8, 2025, Rehema alisema kuwa NSSF inaendelea kufikisha elimu kwa wajasiriamali kuhusu umuhimu wa kujiunga na mfuko huo ili kujiwekea akiba kwa maisha ya sasa na ya baadaye.
Alibainisha kuwa kuna njia mbili za kujiunga na NSSF. Moja ni kwa kujaza fomu, na nyingine ni kutumia mifumo ya kidijitali kwa wale wenye namba za NIDA. Wanachama wanaweza kuchangia michango yao kupitia simu za mkononi wakiwa popote walipo. Kima cha chini cha uchangiaji ni shilingi 30,000, ambapo mwanachama atanufaika na fao la matibabu pamoja na mafao mengine.
Baadhi ya wajasiriamali waliojiunga na NSSF walielezea manufaa wanayopata kwa kuwa wanachama wa mfuko huo. Pastory Anthony, mmoja wa wanachama wa NSSF, alisema kuwa ananufaika na mafao ya matibabu kwa familia yake na yeye binafsi. Alitoa wito kwa wajasiriamali wengine kujiunga na NSSF ili kujihakikishia usalama wa kifedha.
MarcDonald Maganga, Afisa Mkuu wa Sekta Isiyo Rasmi, alifafanua kuwa NSSF imeweka utaratibu mzuri wa kuwahamasisha wajasiriamali kujiunga na mfuko huo. Alieleza kuwa baada ya kujiandikisha, mwanachama hupewa namba ya kumbukumbu ya malipo na anaruhusiwa kuchangia kuanzia shilingi 30,000, 52,200 au zaidi kwa mwezi.
Aidha, mwanachama anaweza kuchangia kidogo kidogo kwa siku, wiki, mwezi, muhula, au msimu kulingana na uwezo wake. Mafao yanayopatikana ni pamoja na fao la uzee, urithi, uzazi, matibabu, na msaada wa mazishi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED