TANESCO wamtibua nyongo Dk. Biteko

By Beatrice Moses , Nipashe
Published at 04:37 PM Jan 09 2025
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko.
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko.

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko ameamuru Kitengo cha Huduma kwa wateja Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kufumuliwa na kupangwa upya, ili kumudu kuwahudumia wateja ipasavyo, ikiwamo kupiga simu za malalamiko bure.

Hayo yametokea leo kwenye ofisi za Kitengo hicho zilizopo Ubungo, Dar es Salaam, ambapo Dk. Biteko alifika hapo ikiwa ni sehemu ya ziara yake.

Dk. Biteko baada ya kufika hapo alipokelewa na uongozi wa Tanesco, ambapo alipata maelezo kadhaa kabla ya kuanza kuwahoji akitaka kujua utekekelezaji wa maagizo aliyowapa mwaka jana (Aprili 2024)ikiwamo kuwa namba maalum ambayo wateja wanaweza kupiga bure, akielezea kukerwa wateja kuingia gharama na kukosa huduma waliyoitarajia.

‘Nikimpigia meneja wa mkoa ndani ya muda mfupi tayari karekebisha, actually nawamini mameneja wa mikoa kuliko nyie hapa, hatuwezi kukubali jambo hili liendelee  tafuteni uongozi mpya muweke hapa ndani ya wiki nataka hapa pasukwe upya nataka nione wananchi wanahudumiwa,”amesema Dk. Biteko.  

Dk, Biteko amesema kuwa anatambua malalamiko yameongezeka kuhusu huduma za Tanesco, ambao wamekuwa wakidai kuwa ni kutokana na mifumo kuwakwamisha.

“Hii mifumo nani anaye manage kwa nini mifumo ni Tanesco tu kwani nini makampuni mengine hayana malalamiko ya mifumo ni Tanesco tu, ‘amesema. 

Ameuagiza uongozi wa Tanesco kukutana na TCRA na kufanya nao mazungumzo ya namna ya kufanikisha namba hiyo kuanza kufanyakazi  ili kuwapunguzia mzigo wa wa gharama wateja wao haraka.