Mradi wa visima Pwani kukamilika Januari 30

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 04:59 PM Jan 09 2025
Mradi wa visima Pwani  kukamilika Januari 30.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mradi wa visima Pwani kukamilika Januari 30.

NAIBU Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, amesema ifikapo Januari 30, mwaka huu, mradi wa visima unaotekelezwa katika Mkoa wa Pwani utakamilika na kufikisha huduma ya maji katika maeneo yaliyolengwa.

Mhandisi Kundo ametoa kauli hiyo alipokuwa katika ziara yake ya kikazi kukagua miradi ya maji inayosimamiwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) na DAWASA katika Wilaya ya Bagamoyo.

Amesema kuwa lengo la Rais Samia Suluhu Hassan, ni kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama karibu na makazi yao, jambo ambalo Mkoa wa Pwani linaendelea kutekelezeka kwa kasi.

“Kuna mradi wa visima unaotekelezwa mkoani hapa, na ifikapo Januari 30, tutakuwa tumekamilisha maeneo yote yaliyolengwa, hivyo kuwaondolea adha wananchi waliokuwa wanapata changamoto ya huduma ya maji karibu na makazi yao,” amesema.

Aidha, amewahimiza wananchi kuitunza miundombinu ya maji ili adha za ukosefu wa huduma hiyo zisijirudie. “Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye miradi ya maji ili shughuli zenu za kila siku zisiathirike. Hii pia ni sehemu ya Mpango wa Rais wetu wa kumtua mama ndoo kichwani, tunautekeleza kwa vitendo,” ameongeza.

Meneja wa RUWASA Mkoa wa Pwani, Mhandisi Beatrice Kasimbazi, amesema mkoa huo unatekeleza mradi wa visima 40 katika majimbo manane. Visima hivyo ni sehemu ya visima 900 vinavyochimbwa katika maeneo mbalimbali nchini.

“Kwa Mkoa wa Pwani, utekelezaji wa mradi huu umefikia asilimia 72. Visima 29 tayari vimeanza kutoa maji, huku visima 11 vikiendelea kukamilishwa. Visima 35 ni virefu vinavyochimbwa, na vitano vinatumia vyanzo mbadala kama mabwawa. Ifikapo Januari 30, visima vyote vitakuwa vimekamilika na kuanza kutoa huduma,” amesema.

Mhandisi Kasimbazi ameongeza kuwa RUWASA inaendelea kutekeleza miradi mingine ya maji, na kwamba ifikapo Desemba mwaka huu, upatikanaji wa maji vijijini utafikia asilimia 88.

Mkazi wa Kitongoji cha Diagala, Kijiji cha Dihozile, kata ya Msoga, Lucy Kilekeni, ameishukuru Serikali kwa kufikisha huduma ya maji, ambayo inakwenda kuwaondolea adha ya kununua dumu la maji la lita 20 kwa shilingi 1,000.

“Kabla ya mradi huu, tulilazimika kutumia maji ya lambo au kununua maji safi kwa ajili ya kunywa, ambayo yalipatikana mbali. Hali hii sasa imebadilika,” amesema Lucy.