Ntobi aliwa kichwa CHADEMA, kwa kumtusi Lissu

By Ambrose Wantaigwa , Nipashe
Published at 01:53 PM Jan 09 2025
 Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi.
Picha: Mtandao
Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi.

KAMATI ya Utendaji ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kanda ya Serengeti wamemvua Uongozi Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi kwa kile kinachoelezwa kuwa ni utovu wa nidhamu dhidi ya viongozi wa chama hicho Taifa.

Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la CHADEMMA Kanda ya Serengeti, Lucas Ngoto amewaambia waandishi wa habari Mjini Tarime leo kuwa maamuzi hayo yamefikiwa kutokana na kauli na maandiko kadhaa ya Ntobi yasiyokuwa na utu na heshima kwa Viongozi wa Chama Taifa.

Amesema kikao kilichoketi Shinyanga jana siku ya Jumatano Januari 08, 2025 wajumbe kwa kauli moja wamethibitisha tuhuma zaidi ya nne ikiwemo kukiuka maadili na kuchafua viongozi wa chama kitaifa kupitia mitandao ya kijamii.

Aidha amesema amekuwa na mfululizo wa maandiko kadhaa, yenye nia ya kumchafua, kumtweza na kumtusi Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu ambaye ni mgombea mwenza wa Freeman Mbowe kwenye nafasi ya Uenyekiti wa CHADEMA Taifa.

Ametaja baadhi ya kauli za Ntobi zilizothibitishwa na wajumbe hao ni pamoja na kumuita Makamu Mwenyekiti Lissu mropokaji na mmbea, na kumtuhumu mara kwa mara kwa mambo ambayo sio ya kweli kinyume na utaratibu na kanuni za chama.

Taarifa ya CHADEMA Serengeti.