HII ni wikiendi nzito kwa wadau wa soka na mashabiki wa klabu za Simba na Yanga ambazo zote zipo ugenini kusaka nafasi ya kusonga mbele kwenye michuano ya kimataifa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Simba, ambayo inashiriki Kombe la Shirikisho Afrika ipo nchini Angola kwa ajili ya mchezo wao wa kesho wa michuano hiyo dhidi ya Bravo do Maquiz ya nchini humo.
Watani zao wa hapa nyumbani, Yanga wenyewe wapo Maritania kucheza na Wasudan, Al Hilal na wenyewe wakisaka pointi tatu zitakazowasogeza karibu kabisa na mlango wa kuingia robo fainali ya michuano hiyo.
Kwa hapa nyumbani mashabiki wa klabu hizo wanasubiri baada ya dakika 90 kwa kila mchezo kuanza kutambiana na kuchekana kwa kile kitakachotokea kwenye michezo hiyo.
Kimsingi klabu hizi zote zinaipeperusha bendera ya Tanzania kwenye michuano hiyo ya kimataifa inayoandaliwa na CAF, kufanya vizuri kwa klabu hizo ni sifa kwa Ligi yetu na nchi kwa ujumla.
Kutokana na namna ya misimamo katika makundi ya timu hizi kwenye michuano hiyo ya CAF ilivyo, kila timu ina nafasi ya kusonga mbele, kikubwa ni kuchanga vyema karata zao.
Tunaamini kila timu ikipambana kikamilifu, wachezaji wakajitoa dakika zote 90 huku wakiweka malengo ya kupata ushindi, hakuna kitakachoshindikana.
Yanga hawapaswi kuangalia matokeo ya timu nyingine, cha kwanza ni lazima washinde kwanza mchezo wao wa kesho kabla ya kuanza kuufikiria mchezo wao wa mwisho dhidi ya MC Alger ambao utachezwa kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa.
Wachezaji wa Yanga wanapaswa kupambana hasa ndani ya uwanja kwenye mchezo wa kesho kuweza kupata ushindi muhimu ambao utaweka hai matumaini yao ya kutinga kwa mara ya pili mfululizo hatua ya robo fainali.
Uwezo wa kufanya hivyo Yanga wanao kikubwa ni kujituma uwanjani katika dakika zote huku pia wachezaji wakifuata maelekezo ya kocha wao.
Kama ilivyo kwa Yanga, Simba nao wana nafasi hiyo ya kupata ushindi na kukata tiketi ya kuingia hatua ya robo fainali Kombe la Shirikisho Afrika.
Utofauti wao na Yanga kutokana na msimamo wa makundi yao, Simba ikipata ushindi kwenye mchezo wa kesho watakuwa wamekata tiketi moja kwa moja kucheza robo fainali bila kusubiri mchezo wao wa mwisho dhidi ya CS Costantine.
Ikumbukwe Simba ina pointi tisa sawa na vinara CS Costantine ambao wao watakuwa wanacheza na 'vibonde' wa kundi, CS Sfaxien, matokeo zaidi ya ushindi yatawafanya Simba nao kusubiri mchezo wao wa mwisho kujua kama watatatinga hatua hiyo ya robo fainali.
Hakuna kinachoshindikana kwenye soka, inawezekana Tanzania ikawa na timu mbili kwenye michuano miwili tofauti katika hatua ya robo fainali.
Kikubwa tunachosisitiza na kushauri, wachezaji wapambane kesho kwa dakika zote tisini kuhakikisha wanapata ushindi huo muhimu ili waweze kutinga robo fainali.
Nipashe tunazitakia kila la heri timu zote tukiamini zinaiwakilisha Tanzania kwenye michuano hii ya CAF, hii itatoa faida kwa Ligi yetu kuzidi kupanda viwango vya ubora miongoni mwa Ligi za Afrika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED