NADHANI sasa tutaanza kuelewana taratibu juu ya wachezaji wazawa na wa kigeni kwenye ligi yetu.
Umekuwa ni mjadala usioisha, kuhusu kupunguza idadi ya wachezaji wa kigeni, waendelee kuwa 12, au waongezwe.
Kuna baadhi wanataka wapunguzwe kabisa, wawe angalau watano au watatu tu ili kulinda vipaji vya wachezaji wazawa.
Hawa wanaona kuwa wachezaji wa Kitanzania hawapati nafasi ya kuonekana kwa sababu kuna idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni.
Mawazo yao ni kwamba wachezaji wazawa wakipata mechi nyingi sana za kucheza watakuwa kwenye viwango vya hali ya juu na kuisaidia timu ya taifa, Taifa Stars au timu ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars.
Wanaona kuwa kuwepo kwa wachezaji 12 wa kigeni, kunaua vipaji vya wachezaji wazawa.
Wapo wanaotaka wachezaji wa kigeni waendelee kuwa 12, waongezeke au kusiwe kabisa na idadi. Nao wana sababu zao. Wanasema idadi inayotamkwa 12 ya wachezaji wa kigeni haifikiwi na timu zote 16 zinachocheza Ligi Kuu. Timu ambazo zina uwezo huo sana sana ni Simba, Yanga, Azam na Singida Black Stars. Zilizobaki zinasajili wachache wachache na zipo ambazo hazina kabisa wachezaji wa kigeni. Hapo wanashangaa ni kwa nini wachezaji wachache tu wa kigeni wanaonekana wanawabana wazawa?
Binafsi naungana na hawa ambao hawaoni shida kuwa na idadi kubwa ya wageni kwenye ligi yetu.
Huwa najiuliza kama wachezaji wa kigeni wanazuia kuonekana kwa vipaji vya wazawa, basi wachezaji wazawa wa klabu za Simba na Yanga wasingeonekana kabisa na kuchaguliwa kwenye vikosi vyetu vya timu ya taifa. Nadhani wachezaji wa klabu ambazo hazisajili wachezaji wa kigeni ndizo zingekuwa na wachezaji wengi Stars. Kwa sababu hawabanwi. Wao wanacheza mechi zote 30 na vipaji vyao vinaonekana.
Nilitegemea klabu kama Mashujaa FC, JKT Tanzania na zingine chache zingekuwa na lundo la wachezaji Taifa Stars au Kilimanjaro Stars kwani hawabugudhiwi na mtu yoyote.
Nilikuwa majiuliza maswali mengi tu, nikasema ipo siku tutajua. Lilikuwa ni suala la muda tu.
Michuano ya Kombe la Mapinduzi ambayo imezishirikisha timu za taifa, imetuonyesha kuwa kwenye soka kinachotakiwa ni kipaji na kujituma, siyo kutengeneza kanuni, au kukataza mtu mwenye uwezo asicheze, ili kumsaidia mwenye uwezo mdogo.
Ni sawa na wazazi kijiji kukataza wanafunzi wenye uwezo mkubwa darasani wasifanye mtihani na watoto wao, wakihofia hawatofanya vyema, badala ya kufurahia kupima uwezo wao.
Timu ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars ilikuwa na wachezaji wengi kutoka klabu ambazo hazibanwi na wachezaji wa kigeni. Hii ilikuwa ndiyo njia ya kuwasuta wanaopenda wachezaji wa kigeni.
Tulitegemea kwa vile wachezaji wa Simba, Yanga na hata Azam hawapo kwenye kikosi cha Kilimanjaro Stars, wachezaji wa timu nyingine zilizobaki wangetumia fursa hiyo kuonyesha vipaji vyao na kuisaidia timu kwenye michuano ya mapinduzi, lakini imekuwa tofauti.
Katika michuano hiyo ya Mapinduzi, Kilimajaro Stars imejikuta ikipoteza mechi zake zote tatu ilizocheza na kuondolewa kwa aibu kwenye michuano hiyo.
Kilichoonekana kuna uzoefu fulani ulikosekana. Tuseme ukweli tu kuwa wachezaji wa Simba, Yanga na Azam wanapata changamoto kutoka kwa wachezaji wa kigeni ambao wanafanya wasibweteke, badala yake wanajituma na kufanya mazoezi kwa bidii ili kupigania namba.
Hilo haliwi faida kwao na klabu zao tu, bali hata kwa timu za taifa kama tulivyoona.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED