Wadau washiriki kikamilifu kutangaza vivutio vya utalii

Nipashe
Published at 08:31 AM Jan 10 2025
 Vivutio vya utalii.
Picha:Mtandao
Vivutio vya utalii.

UTALII ni sekta muhimu katika mchango wa pato la taifa kutokana na Tanzania kujaliwa kuwa na vivutio mbalimbali kama vile mbuga za wanyama, fukwe na mambo ya kale. Sambamba na vivutio hivyo, kuna maeneo mbalimbali ya kihistoria kama vile ya biashara ya utumwa na vita dhidi ya wakoloni ambayo ni chachu katika kukuza sekta hiyo.

Kwa sasa sekta ya utalii pamoja na maliasili, vinachangia asilimia 21.5 ya pato la taifa, hali inayoonyesha kuwa ni mhimili mkubwa katika maendeleo ya nchi kiuchuni. Utalii pekee, kwa mujibu wa takwimu, unachangia asilimia 17.2 wakati asilimia 4.2 inatokana na misitu na nyuki. 

Mbali na pato ghafi la taifa, maliasili na utalii zinachangia asilimia 30.9 ya fedha za kigeni, asilimia 25 zikiwa katika utalii na asilimia 5.9 misitu na nyuki. 

Kwa takwimu hizo inaonesha kuwa sekta hiyo inachangia pia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya uchumi na kupunguza umaskini miongoni mwa wananchi hasa vijana na wanawake kwa kutoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja. Kwa maneno mengine, utalii ni chanzo kikubwa kwa ajira, hivyo kusaidia katika kupunguza umaskini wa hali na wa kipato. 

Kutokana na sekta hiyo kuwa  na mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi,  baada ya kuingia madarakani mwaka 2021, Rais Samia Suluhu Hassan alichukua hatua madhubuti katika kuhakikisha inakua na kuongeza pato la taifa na fedha za kigeni. Kwa kufanya hivyo, Rais Samia kwa kushirikiana na Rais wa Zanzibar, alicheza filamu ya The Royal Tour kwa ajili ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyoko pande mbili za Muungano. 

Baada ya kuchezwa kwa filamu hiyo, kumekuwa na ongezeko la watalii wanaofika nchini kutembelea vivutio mbalimbali zikiwamo mbuga za wanyama na fukwe mwanana zilizoko katika pwani ya Bahari ya Hindi na visiwa za Unguja na Pemba. 

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya maliasili na Utalii Mei, 2024, aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo, Angellah Kairuki, alisema idadi ya watalii kutoka mataifa mbalimbali imeongezeka kutoka 922,692 mwaka 2021 hadi 1,808,205 mwaka 2003. Aidha, watalii wanaoingia nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) waliongezeka kutoka 780,000 hadi 927,000 kwa ajili ya kutembelea hifadhi mbalimbali za taifa ikiwamo kupanda Mlima Kilimanjaro.   

Pia alisema watalii waliotembelea vivutio mbalimbali waliongezeka katika kipindi hicho kutoka 788,933 hadi 1,985,707 sawa na asilimia 152. Ongezeko hilo pia lilichangia kupaa kwa mapato ya fedha za kigeni kutoka Dola za Marekani bilioni 1.3 hadi bilioni 3.4 sawa na asilimia 161. 

Kuwapo kwa hali ya utulivu na usalama ni moja sababu za ongezeko la watalii hao na hivi karibuni Bodi ya Utalii Tanzania imetiliana saini mkataba wa kutangaza vivutio  vilivyoko nchini na Shirika la Ndege la Uturuki katika miji 350 duniani.  Hatua hiyo pia itaongeza wigo wa watali kuingia nchini na kutembelea vivutio na hatimaye kuongeza pato la taifa na maendeleo ya Uchumi kwa ujumla. 

Katika kuhakikisha vivutio hivyo vinaendelea kutangazwa, wadau mbalimbali wanapaswa kushiriki kikamilifu kukuza utalii ikiwamo kuibua vivutio na maeneo ya kihistoria ambayo yatasaidia kuwa chachu kwa utalii na maendeleo ya nchi. 

Ni wazi kwamba kuna maeneo mbalimbali yakiwamo yenye mbuga za wanyama ambayo hayatafikiwa na watalii wengi, hivyo ni wajibu wa serikali na wadau wakiwamo sekta binafsi kuibua vivutio hivyo ili kuendeleza sekta ya maliasili na utalii nchini.