DIRISHA dogo la usajili kwa timu za Ligi Kuu Tanzania Bara, Ligi ya Championship, First League, na Ligi ya Soka la Wanawake, linatarajiwa kufungwa Jumatano wiki hii.
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), limekumbusha kuwa hakutakuwa na muda wa ziada kwa ajili ya usajili. Januari 15 saa 5:59, ndiyo utakuwa mwisho wa kutuma majina kwenye mfumo wa TMS na baada ya hapo hakuna timu yoyote itakayoruhusiwa kufanya hivyo.
Kwa maana hiyo timu inaweza kuwa na mchezaji, imeingia naye mkataba, lakini ikashidwa kumtumia kama itakuwa haijamwingiza kwenye mfumo kwa wakati uliowekwa.
Nimeona timu nyingi ziko kwenye pilikapilika za kusaka wachezaji ambao wanaona watawafaa katika kuboresha vikosi vyao kuelekea mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.
Pia nimeona taarifa, tambo na shamra shamra ya kusajili wachezaji wapya, lakini hili liendane na kuwahi kuwaidhinisha.
Imekuwa ni kama kawaida au mazoea, klabu za soka hapa nchini kukimbizana dakika za mwisho kuingiza wachezaji kwenye TMS, dakika chache kabla ya kufungwa.
Ndiyo muda ambao viongozi wa klabu wanakuwa wamejazana kwenye korido za TFF, kufanya kila linalowezekana ili mradi siku hiyo majina yote ya wachezaji yatumwe.
Nadhani ifike wakati klabu ziondokane na tabia hii, badala yake ikifika Januari 15 kuwe na utulivu, huku klabu chache tu ndiyo zibaki kumalizia, badala ya kuwa na hekaheka kwenye mtandao wa TMS kiasi kwamba mfumo unazidiwa.
Madhara ya mfumo kuzidiwa inajulikana. Ni kwamba majina yaliyotumwa hayaingii katika muda uliokuwa unatakiwa, hivyo baadaye kunatakiwa kuwa na uhakiki wa hali ya juu kujua kama yalitumwa kwa muda sahihi au la. Hapo sasa mchezaji hawezi kucheza mpaka uhakiki ufanyike.
Kinachoonekana ni usumbufu mkubwa kwa viongozi wa klabu kuanza kutuma majina siku ya mwisho ya usajili kwani kuna matatizo mengi yanaweza kujitokeza na kuzima usajili wote.
Majina yatakapotumwa mapema hata kama kuna makosa yanayojitokeza kunakuwa na muda wa kuyatatua kabla ya kuyamaliza, tofauti na yakitumwa wakati wa mwisho.
Mbali na mlolongo wa majina mengi kutumwa siku ya mwisho kiasi mpaka mfumo unalemewa, pia tumekuwa tukiona hata baadhi ya timu zikiweka pingamizi kwa wachezaji hao.
Badala yake TFF inaamua klabu kwenda kumalizana. Inaweza kuchukua wiki moja, mbili mpaka mwezi kufanya hivyo. Ni kipindi ambacho mchezaji inabidi akae bila kucheza, hivyo pia ni hasara ya klabu ambayo imesajili mchezaji aliyetakiwa kuisaidia timu.
Haya yote yanaweza kuepukika kama majina yakitumwa mapema. Kwa maana hiyo nazishauri klabu za soka nchini kuwa huu ndiyo muda wa kutuma majina kabla ya kesho kutwa, ili kuepuka hiki ambacho nimekibainisha hapa. Mtakuja kunishukuru baadaye.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED