MICHUANO ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), kwa timu za wasichana chini ya miaka 17 (Girls Integrated Football Tournament- GIFT), Ukanda wa CECAFA, iliyoanza kutimua vumbi nchini tangu Januari 7, inatarajiwa kutamatika Januari 18, mwaka huu, huku timu inayolelewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), TDS Girls Academy, ikiwa tayari imetinga fainali.
Ilitinga fainali juzi baada ya kuichapa Aigle Noir ya Burundi mabao 2-0, katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam inapofanyika michuano hiyo.
Jumla ya timu nane zinashiriki michuano hiyo. Timu hizo ni Kenya Elite Junior Academy, KAS, JKT Queens, City Lights ambazo zipo Kundi A, na TDS, Boni Consilli Girls, Aigle Noir FC na Hilaad FC, zipo Kundi B.
Ukitazama hapo utagundua kuwa timu nyingi hapa ni za kutoka nje ya nchi, vituo vya michezo, pamoja na shule za sekondari.
Ajabu iliyopo kwenye michuano hii ni kwamba pamoja na kuchezwa hapa nchini, lakini ni JKT Queens ndiyo timu pekee ya Ligi Kuu iliyopeleka timu yake ya vijana kwenye michuano hiyo.
Kwa ujumla tulitarajia kabla ya michuano hiyo, kungekuwa na mashindano ya timu za vijana za U-17 kutoka zile za Ligi Kuu ya Wanawake nchini, Simba Queens, Yanga Princess, Mashujaa Queens, Bunda Queens, Ceasiaa Queens, Alliance Girls, Mlandizi Queens, Get Program, Fountain Gate, Princess na JKT Queens zikichuana vikali ili kuwania nafasi ya kushiriki michuano hiyo ya GIFT.
Kama Klabu ya Aigle Noir, imeweza kumudu kuwa na timu ya U=17 ya wasichana kwa ni nini timu kongwe za soka nchini Simba na Yanga zishindwe? Hii ina maana hazina wachezaji wa umri huo kwenye vikosi vyao zaidi ya vikosi vya wakubwa tu.
Hii haileti picha nzuri kwenye kukuza soka la wanawake nchini, badala yake klabu zetu zinaendelea kutumia na kusajili wachezaji kutoka nje ya nchi na wale wa ndani wengi wakiwa hawajapita njia sahihi ya kulelewa kisoka.
Hapa tunaona nchi kama Kenya na Burundi zimeleta wasichana wao chini ya miaka 17, na nchi hizo zina wachezaji wengi katika klabu za Ligi Kuu soka Wanawake, hivyo wanazidi kujitengenezea mazingira mazuri kwa klabu zetu kuwatupia macho baadaye.
Hatukatai wala kukataza klabu kusajili wachezaji kutoka nje ya nchi, lakini ifike wakati zianze kufikiria kuwa na timu za vijana kwa wanawake kwa faida yao na nchi kwa ujumla.
Soka la wanawake kwa sasa linakuwa kwa kasi, na imeonekana kuwa soko lao ni rahisi zaidi kuuzika kuliko wanaume.
Klabu ikiweza kutengeneza wachezaji wa kike vizuri, haihitajiki mpaka apitie timu kubwa ili auzike nje ya nchi, ni kiasi cha kuonekana ana uwezo mzuri tu, kucheza Ulaya wala si kazi kubwa kama ilivyo kwa wanaume.
Tumeona wachezaji kama Aisha Masaka, Opah Clement, ambao walicheza nchini, hawakuchukua muda kucheza soka la kulipwa Ulaya, hivyo ni wakati wa klabu nchini kujipambanua na kuwekeza pia katika soka la wanawake.
Tunavikumbusha hata vituo vya akademi kuwa biashara kubwa ya kutengeneza wachezaji na kuwauza haraka nje ya nchi kwa sasa ipo kwa soka la wanawake.
Klabu za Ligi Kuu, zikiwamo za Simba na Yanga, zinatakiwa kuwekeza pia kwa nguvu kwenye soka la wanawake kwa kuwa na timu za chini ya miaka 17 na 20, kwani hawatochukua muda mrefu kabla ya kupata faida.
Tunatambua kupata wachezaji wa kike wa umri huo pia ni kazi, lakini pakiwapo na dhamira ya kweli hilo linawezekana na faida kubwa itaonekana mapema, badala ya kusubiri vipaji kuanza kuonekana vyenyewe.
Sisi tunataka kuona mashindano yajayo ya GIFT tunapeleka timu za U-17 ambazo zitakuwa zimeshindana ndani na kupata nafasi hiyo badala kuzitegemea tu JKT Queens na TDS ambazo zina timu za wanawake za vijana.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED