Vitendo vya rushwa ni aibu kwa Jeshi la Polisi, sasa vikomeshwe

Nipashe
Published at 08:04 AM Jan 17 2025
Vitendo vya rushwa ni aibu kwa Jeshi la Polisi, sasa vikomeshwe.

MOJA ya habari kubwa zilizotikisa juzi na jana katika vyombo vya habari ni askari wawili wa usalama barabarani (trafiki) walioonekana kwenye mitandao ya kijamii wakidaiwa kupokea rushwa kutoka kwa baadhi ya madereva wa mabasi ya abiria, maarufu kama daladala.

Askari hao, kwa mujibu wa video hiyo, walikuwa wanasimamisha mabasi hayo kwa madai ya kukiuka sheria za usalama barabarani katika moja ya vituo mkoani Dar es Salaam. Kwa mujibu wa video hiyo, kila dereva au kondakta aliyekuwa akishuka kutoka kwenye basi, alikuwa akimshikisha askari kitu kinachodhaniwa kuwa ni fedha.

Kutokana na tuhuma hizo, juzi, Jeshi la Polisi kanda maalum ya Dar es Salaam, kupitia Kamanda wake, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Jumanne Muliro, lilitoa taarifa kuwa askari hao wameshakamatwa na wamewekwa mahabusu huku taratibu zingine za kinidhamu, zikiwamo kuhojiwa zikiendelea. Kamanda Muliro alisema hatua za kinidhamu za mashtaka ya kijeshi zimeshaanza kuchukuliwa dhidi yao wakati  wakisubiri hatua zingine za kisheria.

SACP Muliro aliongeza kuwa, askari hao walifanya kitendo hicho, wakati  wakitekeleza majukumu yao jambo ambalo ni kinyume cha maadili, hivyo  kuchafua taswira ya Jeshi la Polisi na serikali.

Kwa ujumla, kama alivyosema Kamanda Muliro, kitendo hicho kimelifedhehesha na kuharibu taswira ya jeshi hilo lililopewa dhamana ya kulinda usalama wa raia na mali zao. Pia kimethibitisha kwamba madai ya kuwapo kwa rushwa ndani ya jeshi hilo ni ya kweli kwa kuwa askari hao wamefanya hivyo katika mazingira ya uwazi kabisa.

Mara kwa mara, viongozi wakuu wa serikali, akiwamo Rais Samia Suluhu Hassan wamekuwa wakikemea mambo kadhaa yanayoharibu taswira ya Jeshi la Polisi yakiwamo rushwa, kubambikia watu kesi, baadhi ya askari kushiriki katika vitendo vya uporaji wa mali za watu, vifo vya mahabusu mikononi mwa polisi. Madai mengine ni baadhi ya askari kutokufanya majukumu yao kwa weledi kwa kutanguliza maslahi binafsi hasa wakati wa upelelezi wa kesi.  

Kuwapo kwa vitendo hivyo, wakati akifugua mkutano wa maofisa wakuu wa polisi  mwaka jana, Rais Samia aliagiza jeshi hilo kujitafakari na kumtaka Mkuu wa Jeshi hilo, Inspekta Jenerali Camillus Wambura, kufanya mabadiliko na kuchukua hatua dhidi ya wanaoharibu taswira ya taasisi hiyo nyeti kwa usalama wa raia na mali zao. 

Vitendo vya askari wa usalama barabarani na wengine kudaiwa kupokea rushwa vimekuwa vikiimbwa miaka na miaka na hata kuwa sawa na hadithi isiyo na mwisho. Katika miaka kadhaa iliyopita ripoti maalumu ya chombo kimoja cha Habari ilionesha kuwa rushwa na usalama barabarani iko kila kona ya nchi na mfumo uliozoeleka katika maisha.  

Aidha, kuota mizizi kwa vitendo hivyo kuwapo kwa madai ya kulindana na pia baadhi ya maofisa wa ngazi ya juu kuwa sehemu ya vitendo hivyo. Kwa maneno mengine, kumekuwa na madai kwamba wakubwa hao hupewa mgawo wa fedha hizo na askari walioko chini yao, hivyo vitendo hivyo kuwa sehemu ya kawaida ndani ya jeshi hilo.

Ikiwa ndiyo kwanza mwaka 2025 umeanza na vitendo hivyo kuonekana hadharani huku video nyingine ikioneshwa kuhusu vitendo hivyo, ni wajibu wa Jeshi la Polisi sasa kuchukua hatua kali dhidi ya askari wanaotuhumiwa au kubainika kujihusisha na mambo hayo. Jeshi lichukue hatua madhubuti zikiwamo kufanya mabadiliko ya askari ndani ya kikosi cha usalama barabarani ambacho ndicho kwa kiasi kikubwa kinahusishwa na tuhuma hizo. 

Ni wazi kwamba kama kuna dhamira ya dhati na ya kweli katika kutokomeza vitendo vya rushwa, hasa vikosi na idara zinazohusishwa na mambo hayo, Jeshi la Polisi bila rushwa inawezekana.