TAKRIBANI wakazi 204 wa Mtaa wa Yombo Dovya, Temeke mkoani Dar es Salaam, wameathirika kwa kubabuka ngozi katika maeneo mbalimbali ya mwili, baada ya kudaiwa kutumia mafuta ya kula yenye sumu.
Wakazi hao wanaonekana kubabuka ngozi na kuota malengelenge sehemu mbalimbali za mwili, maumivu makali ya kichwa, kutapika na kuharisha.
Wakizungumza jana Dar es Salaam, baadhi ya wakazi hao walisema wameathiriwa na mafuta na kwamba walianza kupata maumivu makali muda mfupi baada ya kula chakula kilichopikwa kwa mafuta hayo.
Mkazi wa Yombo Dovya, anayefanya biashara ya chapati, ambaye hakutaja jina lake, alisema alinunua mafuta ya kupikia dukani ambayo aliyatumia kukaanga chapati kama kawaida ambazo hata yeye alikula.
“Nilipomaliza kufanya biashara, nikachukua chapati mbili nikala.Ilipofika saa9:00 alasiri, nikaona mabadiliko makubwa sana kwenye mwili wangu. Kikaanza kichwa, shingo haipinduki na mdomoni vidonda tayari vikawa vimetoka,” alisema.
Mkazi mwingine, alisema alinunua chapati kwa mama huyo na muda mfupi baada ya kula, alianza kupata maumivu makali ya kichwa hali iliyomlazimu kulala.
“Hali ilivyokuwa mbaya nikaenda kununua maziwa, nikanywa. Baada ya kunywa tu nikaanza kutapika nikahisi kabisa kwamba hii itakuwa sumu,” alisema.
Mkazi mwingine, alisema mafuta hayo yamewaathiri zaidi watoto ambao wametapika na kuharisha pamoja na kubabuka ngozi, maumivu makali ya kichwa na kupata vidonda kama malengelenge.
Muuzaji wa mafuta hayo aliyetajwa kwa jina moja la Kamau maarufu kama Mangi, alisema alipokea malalamiko ya wateja kuumwa baada ya kutumia mafuta anayouza, jambo lililomlazimu kuyabadili na kuuza dumu lingine, lakini hali ya wateja haikubadilika.
“Mafuta niliagiza kama madumu 20 hivi, nikawa nauza kama kawaida. Nikapokea changamoto kutoka kwa wateja na sikupuuza. Nikayarudisha kwenye dumu, nikafungua dumu jipya, lakini malalamiko hayakuisha,” alisema.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Dovya, Denis Moyo, alisema alipokea taarifa za maumivu yaliyosababishwa na mafuta ya kula, ndipo alipochukua hatua ya kuwapeleka Kituo cha Afya, kwa uchunguzi.
“Tumeingia kila nyumba, Kitongoji chote hiki, tumebaini jumla ya watu 204 wenye dalili za moja kwa moja za matatizo haya. Tukiwauliza, mwingine anasema alikula chapati, mwingine kitumbua, maandazi, chakula au chipsi,” alisema Moyo.
Akizungumza na Nipashe jana, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, alisema tayari ameunda timu kuchunguza mafuta hayo na kwamba muuzaji wa jumla aliyetajwa kwa jina la Ali Hafidh ‘Mpemba’, amekamatwa.
Alisema uchunguzi wa awali umebaini kwamba madumu ya mafuta hayo, hayana ‘seal’.
“Tulikuta madumu 99 hayana seal, alipoulizwa sababu za madumu hayo kutofungwa vizuri alisema wanapoyanunua jumla wanaondoa seal ili wasafirishe vizuri,” alisema Mapunda.
Alisema maelezo hayo yameongeza mashaka na kwamba madumu hayo yamezuiwa ili kufanyiwa uchunguzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na muuzaji huyo anashikiliwa na vyombo vya dola.
Alisema wananchi walioathirika wameshatibiwa na kuruhusiwa na kwamba kinachosubiriwa hivi sasa ni taarifa ya TBS ili kubaini kiini cha tatizo la mafuta hayo.
“Wananchi wametibiwa na wote wamesharuhusiwa kurudi nyumbani,” alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED