Makandarasi wanaovurunda kazi sasa wachukuliwe hatua

Nipashe
Published at 08:32 AM Jan 16 2025
Makandarasi.
Picha:Mtandao
Makandarasi.

KWA miaka mingi, makandarasi wazawa wamekuwa wakilalamika kutokupewa kazi za mradi mbalimbali ya ujenzi na badala yake wanaopewa kazi hizo ni wale wa kutoka nje.

Matokeo ya kukosa kazi hizo, kwa mujibu wa makandarasi hao ni kuendelea kuwa katika hali duni na kushindwa kuchangia pato la taifa kwa kushindwa kulipa kodi na kupata fedha za maendeleo yao.  

Pamoja na kilio hicho, serikali kwa awamu tofauti, imekuwa ikiwajibu kuwa sababu kubwa kwa makandarasi hao kukosa kazi ni uwezo mdogo kwa maana ya teknolojia na kifedha kulinganisha na wale wa nje.  

Pia makandarasi hao walikuwa wakikosa fursa hizo kwa kuwa mazingira yaliyokuwapo hayakutoa nafasi kwao kupata mikopo katika taasisi za fedha kwa sababu mbalimbali. 

Wakati fulani, aliyewahi kuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Magufuli, akiwa Waziri wa Ujenzi, aliwatania makandarasi hao kuwa baadhi yao hawaaminiki kwa kuwa fedha zao hazielekezwi katika miradi na kujiendeleza badala yake wanazitumia kwa anasa ikiwamo kuoa wake wengi. Pia alisema ubinafsi ni sababu nyingine inayowanyima miradi kwa sababu badala ya kuungana ili wafanye kwa viwango, kila mmoja anataka afanye peke yake ili apate fedha zote.  

Kutokana na kuwapo kwa hali na mazingira hayo, serikali kupitia Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), ilianza kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo makandarasi ili kufikia hatua ya kupewa kazi mbalimbali za ujenzi na hatimaye kupunguza kilio chao cha kunyimwa miradi. Pia baadhi ya taasisi za fedha zilianza kuwajengea uwezo makandarasi hao kwa kuwapatia mikopo ili kujiendeleza na kuwa na ukwasi utakaowapa sifa za kupata kazi.  

Matokeo ya mambo hayo ni kwamba makandarasi wazawa walianza kupewa kazi za miradi ikiwamo ya ujenzi wa miundombinu ya shule, barabara, maji na usambazaji wa umeme vijijini chini ya Wakala wa Umeme Vijijini. Baadhi ya waliopewa miradi hiyo katika baadhi ya maeneo walifanya kwa ufanisi lakini wako ambao wameendelea kuvurunda na hata serikali kutishia kutowapa kazi hizo.           

Mfano mzuri ni katika miradi iliyokaguliwa na kuwekwa mawe ya msingi wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru ambao umekuwa ukikimbizwa kila mwaka. Katika baadhi ya maeneo miradi mbalimbali imekuwa ikikataliwa na kutokuwekewa mawe ya msingi au kuzinduliwa kwa sababu ya ama kujengwa kwa kiwango duni au kushindwa kutekelezwa kwa muda uliopangwa kwa mujibu wa mkataba pamoja na kulipwa takribani fedha zote.  

Mbali na miradi hiyo, mingine ikiwamo ya maji, imekuwa ikizinduliwa kuonesha kuwa wananchi wameondokana na kero iliyokuwa ikiwakabili kwa muda mrefu lakini baada ya kitambo kidogo, maji hayatoki kana kwamba yalitegeshwa kumwonesha mgeni rasmi kwamba yapo.    

Aidha, juzi kwa mfano, Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Matthew Kundo, alikataa kuweka jiwe la msingi la mradi wa maji wa Vwawa-Mlowo mkoani Songwe, unaotekelezwa na mkandarasi mzawa, kampuni ya Current Construction Ltd ya Dar es Salaam hadi kasoro mbalimbali zilizojitokeza zitakapopatiwa ufumbuzi.  

Katika mradi huo ambao unatarajia kunufaisha zaidi ya wananchi 23,000 wa kata sita katika wilaya ya Mbozi, ubora wa utekelezaji wake umeibua maswali kutoka kwa naibu waziri huyo, licha ya mkandarasi kulipwa Sh. bilioni 1.3 hadi sasa.

 Miradi kama hiyo iko mingi na imesababisha makandarasi wazawa ambao kwa miaka mingi walikuwa wakilia kukosa kazi, sasa wanavurunda na kuifanya serikali ifikirie vingine kwa sababu ya kutumia mabilioni ya shilingi ambayo yanapotea kwa kazi sizizo na ubora.  Ufike wakati sasa watu kama hao wachukuliwe hatua stahiki zikiwamo za kisheria.