Shule zinapoanza, anza na usalama

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:31 AM Jan 15 2025
Shule zinapoanza,  anza na usalama.
Picha: Mtandao
Shule zinapoanza, anza na usalama.

SHULE za msingi na sekondari zimefunguliwa wiki hii hivyo suala la watoto kusoma, kufurahia shule katika miundombinu bora pamoja na kufaulu ni kipaumbele, lakini usalama wa watoto na ulinzi wao ni jambo linalohitaji wazazi, walezi na jamii kulipa umuhimu wa kipekee.

Kumbukeni pia kuwajali na kuwalinda zaidi wenye mahitaji maalumu wasiiona, wasiosikia, wenye ualbino na ulemavu mbalimbali wa viungo.

Ulinzi na usalama unagusa kila mmoja kuwaangalia kuanzia shuleni wanaposoma, mitaani wanapokaa na mambo muhimu wanayohitaji ili kuwasaidia wasome salama, wasinyanyaswe kijinsia hata kuuliwa.

Lakini juhudi hizi ziende pamoja na kuziweka  huduma za kijamii kama maji, chakula na mabweni shuleni maana vitu hivyo vinapokosekana huleta shida hasa kwa mabinti ambao wanatumbukizwa kwenye mitego na kukwama kimasomo.

Ni kwa sababu watoto wengi wanaoathirika na ukatili wa kijinsia hasa mabinti kupewa mimba utotoni, kutumiwa kingono na walimu au walezi na hata kuozwa kunaweza kuchangiwa na ukosefu wa huduma za jamii.

Ukiangalia zaidi eneo la sekondari, huduma muhimu zinazozungumziwa hapa ni kama chakula, mabweni, maji, hospitali na usafiri.

Kwa kiasi fulani ukosefu wa bweni huwalazimisha wasichana kupanga nyumba mitaani, wakati mwingine kuishi bila maji kunachangia kujihimu alfajiri kwenda kisimani au mtoni au usiku wa manane kusaka maji yote yakiwatumbukiza kwenye mikono ya wanyanyasaji.

Kusoma pasipo na chakula kunamaanisha njaa isiyovumilika, matokeo yake ni binti kufanya lolote bila kujali itakuwaje ili apate chakula, asife njaa. 

Yote hayo na mengine mengi huchangia mimba, utoro na watoto kuchukia shule, kuteswa na kumaliza shule bila kujua kusoma wala kuandika.

Ni vyema wazazi, walezi na wadau wa elimu watatue matatizo hayo yanayohusiana na huduma za msingi ili kupunguza tatizo linalohusiana na kukwamishwa kusoma kutokana na matatizo hayo kila mwaka.

Usalama na ulinzi wa watoto unakwenda mbali zaidi kwa kuwasimamia na kuwaepusha na athari za utandawazi ni kwa sababu umewaharibu watoto wa sekondari na msingi  kwa vile wamekuwa wateja wa mitandaoni kujifunza ‘maovu.’

Wanatumia simu kuangalia picha kwenye YouTube zenye maudhui ya ngono, kujifunza masuala mengine makubwa kuliko mri wao, wapo wanaojifunza na kufanya uhalifu.

Utandawazi unawatumbukiza katika kupenda muziki wa disko usiku, lakini wale wanaokaa mbali na nyumbani au waliopanga mitaani ni wapenzi wa mikesha ya harusi na ngoma.

Wakati mwingine ni waraibu  wa sinema zinazoonyeshwa kwenye mabanda mitaani kama yanavyojulikana kama vibanda umiza.

Wapo wanaocheza kamari, kunywa pombe, kwenda kwenye vijiwe zinapouzwa na kuvutwa bangi. Afya yao kwenye elimu inaporomoka na huenda wakaghadhabika siku ya mtihani wa kuhitimu na kuanza kuandika matusi na kuchora picha za ajabu.

 Watoto hawa wanapokosa uangalizi wanaweza kuishi kwenye nyumba za sinema mchana au vibanda umiza, mabinti wanaweza kuzamia kwenye mikesha au wakaranda mitaani kwa maelezo kuwa hakuna mabweni shuleni wanalazimika kupanga.

Wengi huishia kushawishiwa na kutumbukia kwenye vitendo vya kuwakwamisha kimasomo.

Watoto wanaingia mitegoni wanapokwenda kwenye mabanda yanakoonyeshwa video mchana na kukutana na watu wanaowalipia kiingilio, kuwapa chips na soda kitakachofuata ni ulaghai na hadaa za ngono, zinazoweza kuwaondoa shuleni, kupata mimba na kuzitoa utotoni na kuambukizwa magonjwa.

Pamoja udanganyifu huo mabinti wanaweza kuingizwa mtegoni na walimu ambao ama kwa kisingizio cha kuwafundisha twisheni au kuwaomba wasaidie kazi za nyumbani wanawabaka au kuwashawishi kuingia kwenye ngono.

Ni vyema kuwaangalia watoto wasiwe waathirika wa kutafuta fedha za kujikimu kwa kulazimishwa kufanyakazi za kuosha vyombo, kutafuta kuni, kufua nyumbani kwa walimu na wanavijiji au wanajamii ili kupata fedha za kuishi na kununua mahitaji ya msingi ya kitaalamu na maisha.

Wazazi, walezi, jamii na asasi za kiraia waanze kufuatilia na kuhoji sababu za wasichana au wanafunzi kuzurura, kufanya mambo yanayokwenda kinyume na taratibu.

Mambo yasiishe hapo taarifa zifikishwe polisi, dawati la jinsia, kwa watendaji wa elimu na hata viongozi wa siasa ili kupata ufumbuzi.

Jamii isikae kimya maana kudhalilisha watoto hakuwezi kukoma kama jamii itaendelea kunyamaza.

Kumbukeni kizazi cha watoto wengi wajinga, wasio na elimu bora, waliopotoka watasababisha kuwa na taifa bovu, duni na masikini miaka ijayo.