Hongera TFF, TPBL kusikia kilio udhamini timu zaidi ya moja

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:03 AM Aug 24 2024
TFF.
Picha:Mtandao
TFF.

ILIANZA kama mzaha. Ilianza minong'ono pembeni juu ya mdhamini mmoja kudhamini timu zaidi ya moja kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

Wadau wanajua soka ni mchezo wa 'fair play', hivyo haitakiwi kuwe na maswali kuhusu haki na usawa kwenye michezo mbalimbali.

Wengi walijikita juu ya Kampuni ya GSM kudhamini zaidi ya timu moja, ambapo wamekita mizizi yake kwa Yanga, huku pia ikiwa na udhamini kwenye klabu zingine za Ligi Kuu.

Wadau hao wa soka wakaenda mbali sana wakasema huko Ulaya, hata kampuni ambayo haijajiweka wala kuwa na timu haiwezi kudhamini timu zaidi ya moja kwenye ligi ya nchi moja.

Mfano, Arsenal, Real Madrid zinadhaminiwa na kampuni moja, lakini ni kwa sababu zipo nchi mbili tofauti.

Kampuni hiyo imeruhusiwa kudhamini timu moja tu nchini England na hairuhusiwi kufanya hivyo katika timu nyingine nchini humo, ndiyo maana ikaenda kudhamini kwenye nchi nyingine.

Sababu ni kwamba kama kampuni hiyo ingedhamini zaidi ya timu moja nchini England, mwisho wa siku ingeweza kuamua au kusimamia matokeo ya timu moja ambayo wao wanaweza kuiteua.

Mfano timu zilizodhaminiwa na kampuni moja zikakutana, halafu moja inahitaji ushindi ili asishuke daraja au inataka kuchukua ubingwa, sidhani kama itakosa pointi tatu.

Ni kwa sababu kampuni inayozidhamini itaweka mkono wake kuhakikisha timu yake moja haishuki daraja kwa ajili ya kuendelea kutangaza, au kupata ubingwa ili kuendelea kukuza nembo yake.

Kwa wenzetu jambo hili wanalichukulia kwa uzito sana, na wenzetu hawafichifichi juu ya uwezekano na timu kupanga matokeo kutokana na kuwa zipo kwenye jamii moja.

Baadaye ukawa mjadala mkubwa kwenye vyombo vya habari, televisheni, redio, vijiwe vya soka na mitandao ya kijamii juu ya kuwa hakuna usawa wowote kwa GSM kudhamini klabu zingine huku timu yake mama ikiwa ni Yanga.

Wakasema angalau hata ingekuwa kampuni huru kama ile ya ndege iliyokataliwa Ulaya kudhamini timu zaidi ya moja, lakini ukweli usiopingika kwamba huwezi kuitenganisha GSM na Yanga.

Kampuni hiyo ndiyo inayoisaidia klabu kuleta makocha, kulipa mishahara ya wachezaji na mambo mengi kadha wa kadha.

Hatujawahi kusikia GSM akilipa mishahara Pamba Jiji, Coastal na timu zingine, ina maslahi na Yanga kuliko klabu zingine.

Mjadala huo mkali ukamuibua Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo ambaye amesema amesikia mijadala hiyo na kuahidi kuifanyia kazi.

"Hizi siku mbili tatu umekuwa mjadala mkubwa, lakini kwa wakati huu tuliokuwa nao hakuna kanuni inayozuia kampuni moja kuweza kudhamini zaidi ya timu moja.

Udhamini ni jambo la kikanuni, madhumuni ya kanuni kwa asilimia 90, yameelekezwa kwenye klabu husika, wachezaji, waamuzi, viongozi, mbali na mijadala iliyoibuka, hakuna klabu yoyote au mdau kuelekea msimu huu, aliyelalamikia hilo kuona kama jambo hilo lina ukakasi," alisema Ofisa Mtendaji huyo.

Hata hivyo, alisema kanuni siyo msahafu, hivyo kama wadau wataona kuna haja ya kuja na kanuni hiyo, milango iko wazi.

Lakini mimi siku zote nimekuwa nikiamini kuwa kanuni siyo msahafu, zinajadilika, zinabadilishika kwa hiyo pale ambapo wadau wataona kuna haja ya kufanya mabadiliko ya kanuni kama ambavyo siku zote tumekuwa tukifanya.

 Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF) na Bodi ya Ligi, sisi ni wasikivu mara zote na ndiyo maana unaweza, ukaona zoezi ambalo lina uwazi na ushirikishwaji mkubwa ni eneo la maboresho ya kanuni kuelekea kwenye msimu mpya jambo ambalo linafanyika katika kila msimu," alisema.

Tunaipongeza TFF na Bodi ya Ligi kwa kuahidi kulifanyia kazi suala hilo na kuonekena ni kweli viongozi wapo kwa ajili ya soka na si maslahi binafsi ya mtu mwingine.

Ni kweli suala hili linatakiwa kufanyiwa kazi kwa sababu hata kama hakuna chochote kinachofanyika, lakini kuweka kanuni tu kwa ajili ya chochote kibaya kinachoweza kutokea huko mbele na kuwepo kuaminiana kati ya klabu moja na nyingine zinazoshiriki Ligi Kuu, pia kuiamini kuwa bingwa wake anapatikana kihalali.