WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ametoa maelekezo mahsusi kwa wizara za Uchukuzi na Kilimo, likiwamo la kulisimamia Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuhakikisha huduma na miundombinu ya treni ya mwendokasi (SGR) inaboreshwa ili mradi udumu kwa muda mrefu.
Akitoa hoja ya kuahirisha Bunge jana, Majaliwa aliitaka wizara hiyo kuendelea kulisimamia kwa karibu shirika hilo na kuhakikisha huduma za treni hiyo zinaboreshwa na miundombinu inaimarishwa.
Alisema Desemba 31, 2023, Rais Samia Suluhu Hassan alielekeza kuanza uendeshaji wa reli ya SGR kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Dodoma ifikapo Julai, mwaka huu, na safari zimeanza kwa kipande hicho.
Alifafanua kuwa katika mwaka wa fedha 2024/25, serikali itaendeleza sekta ya uchukuzi kwa kusimamia sekta ya reli ikiwamo ujenzi wa SGR na uendeshaji wa treni ya kisasa ya abiria Dar es Salaam-Dodoma.
Alisema treni hiyo inaendelea kutoa huduma kwa wananchi na imechangia kuimarisha sekta ya usafirishaji.
Majaliwa pia aliiagiza Wizara ya Kilimo isimamie kwa ukaribu upatikanaji na usambazaji wa pembejeo za kilimo hususani mbolea, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu ujao wa kilimo na kwa kuzingatia jiografia za kanda za kilimo nchini.
Kadhalika, aliwataka maofisa ugani waendelee kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi ya teknolojia bora za uhifadhi wa mazao ya chakula na matumizi sahihi ya chakula hicho katika ngazi ya familia.
Kuhusu Rais Samia kuwa Rais Bora Afrika 2023, Majaliwa alisema ametajwa baada ya kuleta mabadiliko makubwa ambayo yameiinua Tanzania na kuing’arisha katika ukuaji wa uchumi, utawala bora na mageuzi ya kijamii.
Alisema Agosti 15, mwaka huu, Jarida la The African Times USA lilimtangaza Rais Samia kutokana na kuvutiwa na jitihada zake za kuleta mabadiliko hayo.
“Jitihada zake za kukuza umoja, demokrasia na uwezeshaji wa wananchi zimekuwa mfano wa kuigwa na viongozi mbalimbali barani Afrika,” alisema.
Alisema Rais Samia ameendelea kujenga miundombinu muhimu na mikubwa ikiwamo ya reli, viwanja vya ndege, mitambo ya kuzalisha umeme na barabara.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED