Waziri Jafo atembelea CBE na kutoa maagizo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:39 PM Sep 06 2024
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo.

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo salaam amekitaka Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), kuwekeza katika ufundishaji wa programu za biashara ya elektroniki zitakazowawezesha vijana kufanya biashara kimataifa.

Alitoa rai hiyo jana jijini Dar es Salaam, alipotembelea chuo hicho katika sehemu ya mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea taasisi zilizo chini ya Wizara yake na kutoa maagizo.

Aliwataka kuendelea kuwa wabunifu kwa kozi zao ili ziende na wakati na kuwawezesha vijana wanaohitimu waweze kumudu kufanya biashara kitaifa na kimataifa na hivyo kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla.

Alikitaka chuo hicho kujikita katika kutoa mafunzo ya kuwajengea maarifa wananchi na watumishi mbalimbali kupitia programu za muda mfupi hali itakayowezesha kuongeza weledi na ufanisi kiutendaji.

Waziri Jafo alikitaka chuo hicho pia kutoa mafunzo ya vitendo zaidi badala ya nadharia ili kuwawezesha wahitimu wa chuo hicho kumudu kujiajiri na kuajiri wenzao mara baada ya kuhitimu.

Alisema serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na  kufanya baishara hivyo chuo hicho kinapaswa kuwaanda wanafunzi kujitegemea wanapohitimu badala ya kuhangaika kutafuta ajira.

Dk. Jafo pia alikipongeza chuo hicho kwa juhudi wanazofanya kuongeza udahili na kupanua miundombinu ya chuo hicho hali ambayo imekiwezesha kuongeza idadi ya wanafunzi mwaka hadi mwaka.

Alisema pamoja na mafanikio makubwa ambayo chuo hicho kimeyapata tangu kuanzishwa kwake lakini bado kinahitaji kuongeza nguvu na kushirikiana na vyuo vingine vya ndani na nje ya nchi ili kufanikisha ndoto za vijana wa Tanzania.

Ziara ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo alipotembelea Chuo cha Elimu ya Biashara CBE jana jijini Dar es Salaam.

“Ulimwengu unabadilika kwa kasi na biashara ndiyo jambo la msingi kwa hiyo tusisitize biashara kwasababu tunataka vijana wetu wafanye biashara kimataifa tuachane na analojia. Lazima vijana wetu wawe na uwezo wa kufanya biashara kielektroniki kimataifa,” alisema Waziri Jafo

Awali,  Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Edda Lwoga aliishukuru serikali ya Tanzania na Zanzibar kwa kuendelea kukisaidia chuo kupata maeneo ya kujitanua na kujenga kampasi zake na kwamba mpaka sasa wamefanikiwa kuwa na kampasi Mwanza, Mbeya, Dar es Salaam na Dodoma.

Alisema kwa sasa chuo kimeanza kutoa maafunzo ya uanagenzi ambapo mwanafunzi anasoma nusu darasani na muda mwingine anautumia sehemu ya kazi ili kumpa ujuzi utakaomsaidia kujiajiri anapomalisa masomo yake chuoni hapo.
Ziara ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo alipotembelea Chuo cha Elimu ya Biashara CBE jana jijini Dar es Salaam.
Alisema kupitia mpango huo wanashirikiana na taasisi na kampuni mbalimbali ambazo zimekuwa zikiwapa fursa ya mafunzo kwa vitendo wanafunzi wa chuo hicho na kwamba matokeo ya program hiyo imeendelea kuwa na mafanikio makubwa.

Alisema chuo kimewajengea uwezo wa kibiashara wajasiriamali wapatao 1,500 kwa mwaka wa fedha 2023/ 24 na kwamba mpango ni kuwafikia wafanyabiashara wengi zaidi ili kuwapa elimu hiyo.

“Tumeshasaini mkataba wa makubaliano baina yetu na Shirika la Viwango Tanzania TBS, Wakala wa Vipimo WMA kuhusu kozi ya metrolojia na tumeshasaini mkataba na serikali mtandao (eGA) kwaajili kutoa  mafunzo ya digital and technology solution,” alisema