WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe amewataka viongozi wa ngazi za juu wa kampuni inayonunua tumbaku katika mikoa ya Katavi, Shinyanga na Tabora, wajisalimishe katika kamati ya uchunguzi kujibu tuhuma wanazohusishwa nazo za uhujumu uchumi.
Viongozi hao wanadaiwa kuwauzia wafanyabiashara magunia ya kufungashia tumbaku badala ya kuyarejesha kwa wakulima ambao ndiyo wamiliki halali wa magunia hayo yanayoitwa "majafa".
Bashe alitoa agizo hilo juzi mjini Tabora wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya operesheni maalumu aliyoanzisha ya kuwasaka wanaofanya biashara haramu ya magunia hayo katika mikoa hiyo.
Pasipo kutaja kampuni hiyo, Bashe alisema kupitia operesheni hiyo, watu 15 wamekamatwa wakiwamo wafanyabiashara, wakihusishwa na majafa hayo yenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 1.8 ambayo yalitakiwa kurejeshwa kwa wakulima ili kufungia tumbaku ya msimu huu wa kilimo.
"Majafa yalikamatwa yakiwa yamefichwa kwa ajili ya kuwauzia tena wakulima kinyume cha taratibu, walipaswa wapewe wakulima kwa kuwa ni mali yao," alisema Bashe.
Waziri huyo alitangaza vita dhidi ya vitendo vya uhujumu uchumi vinavyofanyika kwenye zao hilo la tumbaku.
Bashe alisema: "Kuna mtandao mkubwa wa watu wanaojihusisha na vitendo hivyo nchini, kwahiyo ninapoanzisha operesheni hii watu wasiingilie kwa kuwa operesheni hizi zimekuwa zinaingiliwa na mambo ya kisiasa kwa sababu huenda ni wanufaika wakubwa wa vitendo hivi vya uhujumu uchumi kwenye zao hili la tumbaku."
Alisema wakulima hao wa tumbaku wamekuwa wanakatwa fedha kila mwaka katika msimu wa kilimo kulipia vifungashio vya majafa na kuwasababishia utitiri wa madeni, wajanja wachache wakiendelea kunufaika huku wakulima wakiendelea kukabiliwa na umaskini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED