MAKAMU wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Othman Masoud Othman, ametangaza rasmi ataomba ridhaa ya Chama cha ACT-Wazalendo kumteua kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Sambamba na hilo, Othman ameweka wazi kuwa vyovyote itakavyokuwa, hata bila Katiba Mpya, ACT - Wazalendo itashiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Alisema hayo jana mjini Unguja alipozungumza na wahariri katika salamu zake za Mwaka Mpya 2025.
"Huu ni mwaka wa uamuzi. Sisi tushiriki uchaguzi. Haijalishi kutakuwa na mazingira gani. Vyovyote atakavyoanguka, ndivyo tutakavyomchinja," alisema.
Alitaja mambo 11 yanayomsukuma kuutaka urais, akisisitiza anaamini yatainusuru Zanzibar kutoka hali ya sasa aliyoita “kuwa nyuma kimaendeleo kulinganishwa na rasilimali ilizonazo”.
Mambo hayo ni pamoja na kudai haki na mamlaka ya kuiwezesha Zanzibar kutumia rasilimali zake kujenga ustawi wa uchumi sawa na hata zaidi ya nchi nyingine za visiwa kama vile Mauritius, Seychelles, Cape Verde; kuwarejeshea wananchi haki ya kuwawajibisha wanaoongoza serikali kupitia uchaguzi huru na wa haki na kujenga misingi ya utawala bora unaojikita katika uwazi na uwajibikaji.
Lingine ni kufanya marekebisho ya mfumo wa kikatiba na kisheria ili kuondoa mamlaka aliyoyaita “ya kifalme kwa Rais” kwa kujenga misingi bora ya kuchungana na kutoa fursa zaidi kwa wananchi kushiriki katika uendeshaji wa nchi yao kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa zilizo imara na zinazowatumikia watu badala ya kuwa mzigo mwingine kwa raia.
Othman alitaja mambo mengine yaliyomsukuma ni kutaka kujenga umoja wa kweli wa kitaifa utakaoakisi utengamano wa kijamii kwa kuimarisha usawa, haki za raia na mshikamano; kujenga mfumo bora na wenye ufanisi wa kupambana na ufisadi wa aina zote na kuzuia matumizi mabaya ya ofisi za umma na rasilimali pamoja na kujenga misingi bora ya uchumi itayotumia vizuri rasilimali za Zanzibar kwa njia endelevu, ukiwamo utalii wenye tija na unaolinda mazingira na nafasi bora na ya kipekee ya kijiografia ya Zanzibar.
Alisema pia anakusudia kuwajengea wananchi fursa ya kushiriki katika uchumi kwa kulinda haki zao za ardhi na nyenzo za kiuchumi; kuwawezesha wote ambao wamefikia kiwango stahiki cha fani mbalimbali ili wakue na kuzalisha bidhaa na huduma katika soko la ndani na nje; kuwawezesha vijana kuajirika na kujiajiri na kuimarisha huduma za ustawi wa jamii zikiwamo elimu, afya na matunzo ya wasiojiweza na hifadhi ya jamii yenye uendelevu.
Othman ambaye ni Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Taifa, alisema katika kipindi cha zaidi ya miaka 30 cha utumishi wake serikalini, amebaini kiini cha matatizo ya Zanzibar ni uwezo dhaifu wa mfumo wa sasa kiutendaji, sera na usimamizi.
Alisema kuwa kutokana na uzoefu wake huo, hata akashika nafasi ya juu katika taaluma ya sheria – Mwanasheria Mkuu wa Serikali, anaamini anaweza kuivusha Zanzibar kutoka katika dimbwi la matatizo yaliyopo, akisisitiza “inahitaji kunusuriwa haraka”.
Alisema ili kuyafanikisha hayo yote, lazima kuwe na utaratibu wa kuhakikisha kuwa kuna uchaguzi huru, wa haki, unaoaminika na wa wazi mwaka huu wa 2025.
Alikosoa mfumo wa sasa wa uchaguzi, akifafanua unakifanya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa na idadi kubwa ya wabunge na wawakilishi katika vyombo vya uamuzi -- bungeni na Baraza la Wawakilishi ambao "wanapigania zaidi maslahi ya chama chao badala ya maslahi ya taifa."
Alitoa rai kwa viongozi wa serikali na CCM kutafakari kwa kina kinachojiri Zanzibar wakati wa uchaguzi. Wasingependa kuona tena vurugu na hata mauaji yaliyoripotiwa katika uchaguzi uliopita.
Aliendelea kukosoa utendaji usiozingatia maadili serikalini, akirejea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Mwaka 2022/23, zote mbili (Zanzibar na Tanzania kwa ujumla) zinabainisha kukosekana nidhamu katika matumizi na usimamizi wa fedha za umma.
Alisema kunaripotiwa hali hiyo ilhali nao ni sehemu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), lakini wao hawana mamlaka ya kuwawajibisha watendaji wanaokiuka sheria na taratibu zilizowekwa, hivyo wanabaki kuwa jicho la wananchi kama ilivyo kwa CAG.
UCHAGUZI SIKU MBILI
Alikosoa Uchaguzi Mkuu kufanyika kwa siku mbili visiwani Zanzibar, akionya kuwa awamu hii hawatokubaliana na utaratibu huo kwa kuwa wamebaini unalenga kufanikisha uporaji ushindi wa vyama vya upinzani.
Pia alisema wanaendelea na mazungumzo na wenzao wa CCM kuhusu hatima ya SUK, akidokeza kuwa wamebaini kukosekana dhamira ya kutekeleza waliyokubaliana wakati wa mazungumzo yaliyofanikisha kuundwa kwa SUK.
"Katika kikao cha mwisho cha Kamati Kuu ni kweli tuliamua tujitoe katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, katika kulizungumzia hili na upande wa pili, zipo ahadi zilitolewa na tunaendelea nazo. Hatujafika mwisho katika mazungumzo haya," alisema.
Othman pia alikosoa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) ya Baraza la Mawaziri kuongozwa na mwenyekiti asiyetoka upinzani, jambo ambalo ni kinyume cha uendeshaji wa Mabunge ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED