Raizini atajwa Kagera Sugar

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:47 AM Jan 04 2025
Razin Hafidh.
Picha: Mtandao
Razin Hafidh.

STRAIKA wa Mtibwa Sugar, ambaye anawaniwa kwa udi na uvumba na Kagera Sugar inayoshiriki Ligi Kuu, Razin Hafidh, ameendelea kuwa tishio katika Ligi ya Championship baada ya kufikisha mabao 11 hadi kufikia raundi ya 14.

Mabao aliyofunga mchezaji huyo kwa kiasi kikubwa yameifanya Mtibwa Sugar kukaa kileleni katika msimamo wa ligi hiyo, ikifikisha pointi 35.

Kwa mujibu wa takwimu iliyotolewa juzi  na Bodi ya Ligi, Raizin anafuatiwa na Abdulaziz Shahame wa TMA aliyefunga mabao tisa huku straika wa zamani wa Azam, Ihefu FC na Coastal Union, Andrew Simchimba, ambaye kwa sasa anaichezea Geita Gold amefunga mabao nane huku  Msenda Amri wa Stand United, Naku James wa Mbuni FC na Seif Adam wa Mbeya Kwanza, wote wakipachika mabao sita kila mmoja.

Habari zinasema Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Melis Medo, ambaye aliifundisha Mtibwa Sugar katika mechi kadhaa ya Ligi ya Championship, amewaambia mabosi wa timu yake anamhitaji Raizin kwa ajili ya kuboresha kikosi chake.

Raizin, kabla ya kuichezea Mtibwa Sugar, amewahi kuichezea Gwambia FC, African Lyon, Coastal Union na Dodoma Jiji wakati zipo Ligi Kuu Tanzania Bara.

Wakati huo huo, vita kali katika ligi hiyo ni ya kuwania nafasi ya pili ambapo Mbeya City imewaengua Geita Gold iliyokuwa ikiishikilia kwa muda mrefu.