KOCHA Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, amekoshwa na kiwango cha wachezaji wake katika mchezo wa juzi wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, akisema hii ndiyo timu niliyokuwa "naitaka na kuihangaikia" tangu mwanzo, huku akiwaambia wapinzani wake kuwa wana bahati ya kutofungwa mabao saba au manane katika mchezo huo.
Akizungumza baada ya mchezo huo uliochezwa, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, ikishinda mabao 3-1, Ramovic, alisema hiyo ndiyo Yanga aliyokuwa akiitaka tangu alipotua kwenye kikosi hicho na amekuwa akihangaika kuipata, lakini sasa anadhani imeshapatikana.
"Tumecheza na timu ngumu, tuliiheshimu kwa kile ambacho ilichofanya huko miaka ya nyuma, naipongeza kwa kutupa mechi ngumu. Tulihitaji pointi tatu kwa hali yoyote ili tuwe kwenye mbio za kufuzu hatua inayofuata.
Hiki sasa ndicho kiwango chetu, hii ndiyo Yanga niliyokuwa naitaka, wachezaji wangu wamejitahidi kuonesha kile ambacho tulichokuwa tukikihitaji hapo mwanzo wakati naingia kwenye timu hii.
Walikuwa na kasi, pumzi, walikaba na kutengeneza nafasi, hawakukata tamaa tangu wakati tupo nyuma kwa bao moja, waliamini kuwa tutashinda mechi," alisema kocha huyo raia wa Ujerumani.
Alisema kwa jinsi timu zote mbili zilivyocheza, anadhani timu yake ilikuwa na uwezo wa kuondoka uwanjani ikiwa imefunga mabao saba au ikishinda 8-1.
"Nina uhakika kama tungekuwa makini tungeweza kuwafunga hata mabao saba au tungeshinda 8-1, tumekosa mabao mengi sana, lakini hiki tulichokipata tumefurahi, tumepambana na kujituma, kikosi kimeimarika sana," alisema.
Hata hivyo, alisema Kundi A, bado ni gumu na lipo wazi kwa timu yoyote kuweza kufuzu, hivyo kwa sasa wanajiandaa kwa michezo miwili waliyosalia nayo.
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa TP Mazembe, Lamine Ndiaye, alilalamika kuwa bao la kwanza ambalo wapinzani walifunga lilikuwa la uonevu kwani, mchezaji wake alikuwa ameumizwa, hivyo mpira ulipaswa kutolewa nje, au mwamuzi kupiga filimbi.
"Mechi tumetizama wote, kipindi cha kwanza tuliikamata, tukapata nafasi, lakini hatukuzitumia. Goli la kwanza mchezaji wangu aliumia, badala ya mpira utolewe nje uliendelea tukafungwa bao la kusawazisha.
Goli la pili na la tatu, yalikuwa ni makosa ya wachezaji wangu wenyewe hawakuwa makini, nawapongeza Yanga, ni mpira," alisema kocha huyo raia wa Senegal.
Yalikuwa ni mabao mawili ya Clement Mzize na moja la Stephane Aziz Ki, ambayo mbali na kuipa timu hiyo ushindi, yaliipandisha hadi nafasi ya tatu ya msimamo, ikifikisha jumla ya pointi nne, na kuivuta TP Mazembe mkiani, ikiwa na pointi mbili.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED