Bilioni 260/- za CSR Bwawa la Nyerere zinaposuasua miaka minne bila uamuzi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:48 AM Jan 05 2025
Bwawa la Kufua Umeme wa Maji la Julius Nyerere (JNHPP)
Picha: Mtandao
Bwawa la Kufua Umeme wa Maji la Julius Nyerere (JNHPP)

ULIPOANZISHWA tu, ulikutana na hoja kinzani kuhusu hatima ya usalama wa mazingira, lakini uongozi wa juu serikalini ukatolea ufafanuzi kuhusu usalama na faida zinazotarajiwa.

Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme wa Maji la Julius Nyerere (JNHPP), uko mbioni kukamilika, ukigharimu Sh. trilioni 6.5 hadi kukamilika kwake.

Hata hivyo, kuna mambo yasiyofaa yaliyohusiana na mradi huo yameripotiwa. Mojawapo ni ucheleweshaji utekelezaji miradi ya kijamii kwa zaidi ya miaka minne yenye thamani ya Sh. bilioni 262.34.

Wakati mahitaji ya kitaifa ni mengi, hata kuilazimu serikali kukopa, fedha za miradi ya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR) zimebaki kwa mkandarasi kwa miaka minne. 

Ni hoja iliyoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kupitia ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka 2022/23.

Katika ripoti hiyo, CAG anabainisha kuwa kifungu cha 2.1.6 cha Makubaliano ya Utekelezaji Miradi ya Kijamii katika utekelezaji mradi huo, kinaelekeza kuwa, makubaliano ya kina yatajadiliwa na kutiwa saini ndani ya mwezi mmoja baada ya kutiwa saini mkataba wa mradi wa Bwawa la Julius Nyerere.

Kwa mujibu wa mkataba huo, kama ilivyoripotiwa na CAG, mkandarasi ataanza utekelezaji miradi ya kijamii ndani ya mwezi mmoja baada ya kutia saini makubaliano ya kina huku ikizingatiwa malipo ya awali yamelipwa chini ya mkataba wa mradi wa Bwawa la Julius Nyerere.

Kwa mujibu wa mkataba wa utekelezaji mradi wa Bwawa la Julius Nyerere, miradi ya kijamii itatekelezwa kwa gharama ya Sh. bilioni 262.34 (ikiwa ni asilimia nne ya bei ya mkataba).

Mkataba wa mradi wa Bwawa la Julius Nyerere ulitiwa saini tarehe 12 Desemba 2018 na makubaliano ya kina ya miradi ya kijamii yalipaswa kutiwa saini tarehe 13 Januari 2019.

Hata hivyo, hadi kufikia tarehe 30 Juni 2023, Mkataba wa Kina wa Utekelezaji Miradi ya Kijamii ulikuwa haujatiwa saini, ikiwa ni ucheleweshwaji kwa zaidi ya miaka minne (siku 1,610).

Kwa mujibu wa CAG, hali hii ilichangiwa na kuchelewa kuanzisha mazungumzo ya kutia saini Mkataba wa Kina juu ya miradi ya kijamii.

dhibiti ana angalizo kwamba, kuchelewa kufikia malengo yaliyokusudiwa kunaashiria hatari ya kushindwa kutekeleza miradi ya kijamii kwa wakati, ikizingatiwa kuwa mradi uko katika hatua ya mwisho za ukamilishaji.

Vilevile, imebainika kuwa, tarehe 16 Desemba 2019, kilifanyika kikao cha majadiliano kuhusu utekelezaji miradi ya kijamii ambapo pande zote zilikubaliana kutekeleza miradi hiyo, hususani ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Dodoma na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Fuga hadi Bwawa la Julius Nyerere.

Hata hivyo, makubaliano haya hayakutiwa saini kutokana na mkandarasi kueleza kuwa miradi iliyopendekezwa haiendani na vigezo vilivyoainishwa katika mkataba wa utekelezaji miradi ya kijamii, kwa kuzingatia aina na utaratibu wa utekelezaji.

Kwa mtazamo wangu, kuna haja kuchukua hatua za kinidhamu na kisheria dhidi ya watendaji wote waliochangia kutokelezwa matakwa ya kimkataba na kisheria, hata kusabisha zaidi ya Sh. bilioni 260 kutonufaisha wananchi; zikabaki kwa mkanadarasi kwa miaka minne.

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambao ndiyo wamiliki wa mradi huo, walipaswa kuwasiliana na Wizara ya Nishati kuhitimisha mvutano kwa kuchagua miradi itakayotekelezwa na mkandarasi.

Pasi na hatua madhubuti kuchukuliwa, kuna hatari mkandarasi akakabidhi mradi wa Bwawa la Julius Nyerere na kuondoka huku wananchi wakishindwa kunufaika na Sh. bilioni 262.34 za uwajibikaji wake kwa jamii (CSR).