Wizara ya Elimu kupima uelewa wa STEM, TEHAMA sekondari

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 05:47 PM Jan 06 2025
Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia Elimu ya Sekondari kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hadija Mcheka
Picha: Grace Mwakalinga
Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia Elimu ya Sekondari kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hadija Mcheka

WIZARA ya Elimu Sayansi na Teknolojia, imesema itaanza utaratibu wa kuwapima na kufanya utafiti wa kufahamu matokeo ya mafunzo waliyoyatoa kwa walimu wa shule za sekondari wa masomo ya hisabati, sayansi, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), kwa kuwatumia wanafunzi ambao watapewa maswali ya kujibu kupima uelewa wao.

Kauli hiyo, ilitolewa leo na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, anayeshughulikia (Elimu), Dk. Charles Mahera, wakati akifungua mafunzo  ya siku tano kwa walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati pamoja na wathibiti ubora kutoka Mikoa ya Simiyu na Mara, yaliyofanyika wilayani Tarime.

Dk. Charles Mahera, amesema kupitia Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP),wanatekeleza afua mbalimbali  ikiwemo utoaji wa Mafunzo  Endelevu ya Walimu Kazini (MEWAKA) kwa walimu wanaofundisha masomo ya Sayansi, Hisabati na Tehama.

Amesema  katika kupima ubora na utekelezaji wa mafunzo hayo, wanaandaa utaratibu wa kuwapima walimu waliopatiwa mafunzo ili kuona tija kwa kuwatumia wanafunzi ambao wataulizwa maswali namna walivyonufaika.

“Serikali inatumia fedha nyingi kutoa mafunzo haya, lengo ni kuwajengea uwezo walimu wa sekondari wanaofundisha masomo ya Sayansi, Hisabati na Tehama mbinu zitakazowasaidia kuongeza uelewa kwa wanafunzi na kupenda masomo haya,” amesema Dk. Mahera.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anayeshughulikia Elimu, Dk. Charles Mahera akifungua mafunzo
Ameongeza  kuwa wanakusudia kutoa mafunzo kwa walimu 40,000 ifikapo Januari 2026 na kwamba hadi sasa walimu 29,328 wamepata mafunzo hayo na kuimarisha ufanisi katika ufundishaji wa masomo hayo muhimu.

“Katika awamu hii, walimu 7,940 wanatarajiwa kufaidika na mafunzo haya, ikiwa ni hatua muhimu katika kuboresha mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji,” amesema  Dk. Mahera.

Mratibu wa Mradi wa SEQUIP, Dkt. Nicholaus Gati,  amesema  kuwa mradi umefanikiwa kwa asilimia 85 ya fedha zilizotengwa na kwamba malengo ya mradi yanajikita katika kuhakikisha wanafunzi, hususan wakike, wanapata elimu ya Sekondari na kumaliza masomo yao kwa mafanikio.

Amesema wamejikita katika kuimarisha matumizi ya teknolojia ya kidigitali (TEHAMA) na kutoa fursa zaidi kwa wanafunzi wa kike ili kushiriki kikamilifu katika elimu ya sekondari.

Mkurugenzi wa Ualimu, Dk. Huruma Mageni, amesema  kuwa kupitia SEQUIP, walimu wamefundishwa kutumia mbinu za kisasa na changamshi ambazo zinakuza ubunifu na ufanisi katika ufundishaji wa masomo ya Sayansi, Hisabati, na TEHAMA.
Washiriki wa mkutano
Mwalimu wa Shule ya Sekondari Tarime, Eliud Myovela, amesema  matumizi ya TEHAMA yataongeza ufanisi katika ufundishaji na kuwezesha wanafunzi kufikia malengo yao kwa urahisi zaidi.

Mthibiti Mkuu Ubora wa Shule kutoka Halmashauri ya Mji wa Bunda, Mwalimu Paulina Makolo amesema   mafunzo hayo yatasaidia kuboresha mbinu zao za ufundishaji na kuongeza ufanisi wa wanafunzi katika masomo ya Sayansi, Hisabati, na TEHAMA.