Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais (TAMISEMI) imeanzisha kampeni ya ugawaji wa vyandarua vyenye dawa bure kwa kila kaya, ikiwa ni jitihada za kupambana na ugonjwa wa malaria.
Afisa Mwandamizi wa Wizara ya Afya, Peter Gitanya, akizungumza leo Januari 6, 2025, kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria (NMCP), amesema kampeni hiyo inalenga kutokomeza malaria ifikapo mwaka 2030. Katika kikao kazi na waandishi wa habari wa Mkoa wa Shinyanga, Gitanya alieleza kuwa vyandarua vyenye dawa milioni 1.5 vitasambazwa mkoani humo, huku kaya zote zikifikiwa.
"Chandarua kimoja kitatolewa kwa watu wawili kwa kila kaya. Zoezi la uandikishaji linaendelea, na kaya ambazo hazitaandikishwa haziwezi kupewa vyandarua," alisema Gitanya. Aliongeza kuwa uandikishaji ulianza Januari 2 na utakamilika Januari 15, huku usambazaji rasmi ukianza Januari 16 kwa kaya zilizoorodheshwa.
Kwa mujibu wa Gitanya, Mkoa wa Shinyanga unashika nafasi ya nne kitaifa kwa maambukizi ya malaria kwa kiwango cha asilimia 16, ikilinganishwa na wastani wa kitaifa wa asilimia 8. Tabora inaongoza kwa asilimia 24, ikifuatiwa na Mtwara (asilimia 20) na Kagera (asilimia 18).
Happines Nania kutoka Wizara ya Afya aliwasihi wananchi kutunza kadi wanazopewa wakati wa uandikishaji ili kuhakikisha wanapata vyandarua. Alieleza kuwa hata wakipoteza kadi hizo, taarifa zao zipo na wanaweza kuhudumiwa katika vituo husika. Alisisitiza matumizi sahihi ya vyandarua na kuvitunza kwa lengo la kudhibiti malaria.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Faustine Mlyutu, aliipongeza serikali kwa juhudi zake za kupambana na malaria. Alitoa wito kwa waandishi wa habari kutumia kalamu zao kuelimisha jamii kuhusu matumizi sahihi ya vyandarua vyenye dawa, huku akionya dhidi ya upotoshaji unaohusiana na usalama wa vyandarua hivyo.
"Vyandarua vyenye dawa ni salama na havina madhara yoyote. Waandishi wa habari ni muhimu katika kusaidia jamii kuelewa hili," alisema Mlyutu.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga, Greyson Kakuru, aliipongeza serikali kwa kuwashirikisha waandishi wa habari katika kampeni hiyo. Aliahidi kwamba waandishi wa habari wataendelea kupeleka ujumbe sahihi kwa wananchi ili kuimarisha mapambano dhidi ya malaria.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED