Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo, amekiagiza Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kuwaangalia wawekezaji wazawa kwa jicho la pekee.
Vilevile, ametoa maagizo kwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Tume ya Ushindani (FCC) kudhibiti bidhaa bandia zinazozalishwa mitaani ambazo zinadumaza jitihada za wawekezaji wa ndani.
Prof. Mkumbo alitoa maagizo hayo jana mjini Babati, alipofanya ziara katika kiwanda cha Mati Super Brands Limited, kinachomilikiwa na mwekezaji mzawa David Mulokozi. Alisisitiza kuwa, "TIC wawekezaji kama hawa muwape jicho la pekee, kila wanachohitaji wapewe ili waweze kufanya uwekezaji wao kwa ufanisi."
Waziri huyo alibainisha kuwa uwekezaji unaofanywa unasaidiwa na upatikanaji wa umeme wa uhakika kupitia Bwawa la Julius Nyerere na huduma za maji safi kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Babati (BAWASA).
Akitaja changamoto ya bidhaa bandia, Prof. Mkumbo alisema serikali inalichukua suala hilo kwa uzito mkubwa. Alisisitiza kuwa TBS na FCC wanapaswa kuhakikisha wanadhibiti bidhaa bandia ambazo zinaathiri uchumi wa taifa na mapato ya kodi.
Aliongeza kuwa ubunifu unaofanywa na mwekezaji huyo unapaswa kuambatana na juhudi za kutoa ajira kwa vijana, jambo linalosaidia serikali katika kupunguza changamoto za ajira.
Kuhusu hoja iliyotolewa na David Mulokozi juu ya athari za mabadiliko ya sera na sheria za kodi, Prof. Mkumbo alitangaza kuwa serikali itaanzisha chombo maalum cha kusimamia masuala yote ya uwekezaji ifikapo Februari mwaka huu. Alisema, "Mabadiliko ya mara kwa mara ya sera na sheria tunazifanyia kazi, na serikali itaendelea kumuunga mkono mwekezaji ili afanikiwe."
Mkurugenzi Mtendaji wa Mati Super Brands Limited, David Mulokozi, alieleza kuwa ulipaji wa kodi umeendelea kuongezeka kila mwaka.
Mulokozi alisema kiwanda chake kina wafanyakazi 269, ambapo 147 ni wa kudumu na 122 wa kawaida. Hata hivyo, changamoto kubwa ni ukosefu wa chupa kutoka Kioo Limited, jambo linalowalazimu kuagiza kutoka Kenya au Omani. Changamoto nyingine ni uwepo wa bidhaa bandia na sheria ya kodi inayowataka kulipa kodi kabla ya uzalishaji.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED