Nani atakuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara ni swali ambalo limekuwa likiulizwa na makada wa CCM na hata wafuatiliaji wa karibu wa siasa nchini, hasa mwaka huu ambao Tanzania itafanya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Jibu la swali hilo linatarajiwa kupatikana kupitia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM uliopangwa kufanyika mwezi huu, lakini kitendawili cha nani atakuwa Makamu Mwenyekiti atakitegua Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan.
Makamu mwenyekiti anayetakiwa kwa wakati huu ni yule ambaye atakuja kufanyakazi ya kuivusha salama CCM katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Anahitajika makamu mwenyekiti mwenye uwezo wa kukabili jukwaa na hadhira yake. Makamu mwenyekiti asiye bubu wala mbabe, asiye mwenye ‘makando kando’, asiyekuwa mbinafsi, mchoyo na ambaye akisema atasikilizwa na kuaminiwa na wanachama na viongozi wenzake wa chama hicho tawala.
Pamoja na majukumu mengine, makamu mwenyekiti atasimamia maadili ndani ya CCM. Ilivyokuwa mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi wa dola, suala la wanachama kuzingatia maadili ni jambo la msingi kabisa maana ulegevu wowote katika hili ni kupata wagombea ambao hawana maadili.
Kwa jinsi mambo yanavyokwenda CCM, inahitaji makamu mwenyekiti mwenye ushawishi kwa umma, mwenye nguvu na mvuto ambaye hatoyumbishwa kwa namna yoyote ile iwe ndani ya CCM au hata nje ya chama hicho.
Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa kipindi cha uhai wake, katika hotuba aliyotoa mwaka 2005 Chimwaga mkoani Dodoma kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM kuteua wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar, alitaja sifa 13 anazostahili kuwa nazo mtu anayetaka kushika nafasi hiyo.
Pamoja na mambo mengine, Mkapa aliwataka wanaCCM wasichague mtu kwa kumpenda, bali achaguliwe kwa sifa. Mkapa akatoa mfano wa bangili akisema hata ikiwa nzuri kiasi gani, kama inabana kwenye mkono haifai.
Je, hao wanaotajwa au kujitaja kuwa wanaweza kushika wadhifa wa makamu mwenyekiti CCM Bara sifa yao ni kama bangili yenye kubana mkononi au isiyo bana? Kwa vyovyote vile, mtu anayefaa kwa nafasi hiyo asiwe mgeni ndani ya CCM, bali awe mwenye kuvifahamu vikao vya chama, katiba, kanuni na miongozo huku akizingatia sera na hali ya kisiasa.
Hadi sasa kuna watu kadhaa wanatajwa na kuzungumzwa kuwa huenda wana sifa za kushika nafasi hiyo kurithi ‘viatu’ vya Komredi Abdulrahman Kinana aliyejiuzulu wadhifa huo mwaka jana.
Miongoni mwa wanaotajwa ni William Lukuvi, Abdulrahman Juma, Mizengo Pinda, Abdallah Bulembo, Paul Kimiti, Dk. Asha–Rose Migiro, Anne Makinda, na Stephen Wassira.
Makala haya yanaangazia wagombea hao ambao na wengine wanaotajwa kuwa na sifa za kumrithi Komredi Kinana aliyewahipia kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho.
Wa kwanza kumuanga zia ni kada wa siku nyingi, Mwenyekiti wa zamani wa Jumuiya ya Wazazi, Abdallah Bulembo.
Kwa wasiomfahamu Bulembo ni kuwa, kada huyo ameshika nyadhifa mbalimbali ndani ya CCM. Amewahi kuwa Mbunge, Mjumbe wa NEC, Kamati Kuu na kwa sasa ni Mshauri wa Rais Mambo ya Siasa na Jamii.
Mwaka 2015, Bulembo alizunguka nchi nzima kumnadi aliyekuwa Mgombea Urais wa wakati huo, Dk. John Magufuli akiwa Meneja wa Kampeni.
Bulembo ni kada wa CCM mwenye msimamo thabiti, asiyekubali kuburuzwa na hababaishwi na jambo. Ilihitaji moyo na usahamilivu kuweza kuwa meneja wa kampeni ya mwanasiasa wa aina ya Magufuli, lakini kwa busara zake na uwezo wake wa kisiasa, Bulembo aliweza kumnadi vyema Rais Magufuli na kufanikisha ushindi wa kishindo wa CCM.
Mbali na uzoefu wa kisiasa na utumishi ndani ya CCM, Bulembo anaonekana kuwa na sifa nyingine ambayo pengine wengine hawana. Sifa kimsingi, ndiyo inayomfanya awe anatajwa na makada wa CCM kuweza kumrithi Komredi Kinana.
Sifa ya ziada ya Bulembo ni kuwa mwanasiasa anayewakilisha mawazo ya rika tofauti ya wazee, kizazi kipya, umri wa kati na mtu anayeweza kuwa kiungo cha wanasiasa wazee na vijana ndani ya CCM na hata katika vyama vingine vya siasa.
Je, ni hulka yake ya kujichanganya na watu wa rika tofauti? Ni haiba yake ya utu uzima, busara mpenda watu na aliye tayari kujitolea ikibidi hata vitu vyake binafsi?
Ni upeo wake mkubwa wa kuona mambo? Ni hoja zake za kisasa? Ni uzalendo wake? Ni upungufu walionayo wanasiasa wengine wanaotajwa kufaa katika nafasi hiyo? Ni kitu gani hasa? Wana CCM wanapaswa kuyatafutia jawabu maswali haya.
Bulembo mwenye umri wa miaka 63, bado anabeba matumaini ya zama za sasa. Hajapitwa na wakati. Ikiwa zama za leo ni za vijana na watu wa umri wa kati. Wapigakura wengi ni vijana na hadhira ya kisiasa imebadilika sana, hivyo anahitajika makamu mwenyekiti wa CCM anayeweza kuyanadi matarajio ya vijana katika ulingo wa kisiasa na zaidi kwenye kampeni za Ucha guzi Mkuu wa 2025.
Bulembo ni muumini wa dhati kabisa wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na Mapinduzi ya Zanzibar, ni mzalendo na ni mwanasiasa mwenye siasa za kati.
Anaonekana pia kuwa mwanafalsafa ambaye amegeuka kuwa tumaini la mabadiliko chanya ndani ya CCM. Anao uwezo wa kusaidia CCM kukabili changamoto za kisiasa kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Changamoto kubwa inayomkabili Bulembo ni misimamo yake isiyoyumba kwani ni mtu ambaye habadiliki kama kinyonga katika jambo mlilokubaliana. Kwa matamshi mengine, Bulembo si kigeugeu, si ndumi lakuwili, balini mwenye msimamo thabiti kwa matendo na maneno.
Wiki ijayo tutaendelea kuwachambua makada wengine wanaotajwa kuwa wanaweza kushika wadhifa wa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara.
Itaendelea.....
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED