TRA yavuka lengo yakusanya Tril. 3.5/-

By Restuta James , Nipashe
Published at 11:37 AM Jan 02 2025
Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuf Mwenda.
Picha: TRA
Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuf Mwenda.

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imevuka lengo la makusanyo ya kodi kwa asilimia 103.52 mwezi uliopita, kwa kukusanya Sh. trilioni 3.587, huku ikiweka maazimio nane ya kuongeza ufanisi wa utendaji wake kwa mwaka 2025.

Aidha, sekta za madini, benki, uzalishaji viwandani na biashara, ndizo zilizowezesha makusanyo hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuf Mwenda, alisema makusanyo hayo yameiwezesha mamlaka hiyo kukusanya Sh. trilioni 16.528 sawa na asilimia 104.7, katika kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2024/2025 cha Julai hadi Desemba 2024.

Alisema makusanyo hayo ni kiwango cha juu kuwahi kufikiwa na TRA, ikilinganishwa na nusu ya mwaka wa fedha 2023/2024, mamlaka hiyo ilikusanya Sh. trilioni 13.9.

“Makusanyo haya ni sawa na ongezeko la asilimia 78.78 toka Sh. trilioni 9.242 zilizokusanywa katika kipindi kama hichi mwaka wa fedha 2020/2021 kabla ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan,” alisema Mwenda.

Kamishna Mwenda alisema kwa Desemba TRA imevunja rekodi kwa kuongeza ukuaji wa mapato kwa asilimia 17.59 kutoka makusanyo ya Sh. trilioni 3.050 Desemba 2023 hadi Sh. trilioni 3.587 mwaka jana.

“TRA imeandika rekodi mpya ya kuweza kufikia na kuvuka lengo la makusanyo kwa miezi sita mfululizo, katika nusu ya kwanza ya mwaka 2024/2025. Wastani wa kiwango cha makusanyo kwa mwezi umeongezeka kwa asilimia 18.80, kutoka wastani wa Sh. trilioni 2.319 mwaka wa fedha 2023/2024 hadi wastani wa Sh. trilioni 2.755 kwa mwezi mwaka huu,” alisema.

Alisema kwa robo ya pili ya mwaka jana (Oktoba hadi Desemba), TRA ilikusanya Sh. trilioni 8.741 sawa na asilimia 104.63, ikiwa ni ukuaji wa asilimia 19.05 ikilinganishwa na Sh. trilioni 7.342, zilizokusanywa kipindi kama hicho mwaka 2023.

Mamlaka hiyo pia imevuka lengo la makusanyo kila mwezi, kwa kuongeza nidhamu ya utendaji na ubunifu kwa watumishi wake na kuhamasisha ulipaji wa kodi wa hiari.

Pamoja na mambo mengine, TRA imefuatilia kwa ukaribu hali ya ufanyaji wa biashara nchini, kwa kusimamia uzalishaji viwandani pamoja na kuhimiza matumizi ya mashine za kielektroniki (EFD).

Kuhusu sekta zilizoibeba TRA, Kamishna wa Walipakodi wakubwa, Michael Muhoja, alisema ni ya fedha ikiongozwa na benki, madini, uzalishaji viwandani na biashara.

Katika makusanyo ya Sh. trilioni 3.587 ya Desemba 2024, Sh. trilioni 1.660 zimelipwa na benki, wakati biashara na tozo za forodha zikichangia Sh. trilioni 1.100 na kiasi kilichobaki kikilipwa na madini pamoja na uzalishaji viwandani.

Alisema ili kuongeza makusanyo, TRA inaweka mkakati wa kuongeza idadi ya walipakodi wakiwamo wadogo, wa kati na wakubwa.

Mamlaka hiyo inaendelea kutekeleza agizo la Rais Samia la kutaka mifumo isomane; na tayari imeboresha mifumo yake miwili ya usimamizi wa forodha (TANCIS) na ule wa usimamizi wa kodi za ndani (IDRAS), ili pamoja na huduma nyingine, kupunguza ukaguzi wa ‘mikono’ kwenye mizigo inayosafirishwa nje ya nchi.

Akizungumzia mfumo wa IDRAS, Kamishna wa Kodi za Ndani, Alfred Mregi, alisema wameongeza sehemu ya kutunza kumbukumbu ya bidhaa zinazozalishwa nchini, ili kurahisha ukadiriaji wa kodi kwa viwanda vya ndani.

Lengo ni kupunguza malalamiko ya wafanyabiashara kubambikiwa kodi, kwa kuwa taarifa zinazoingizwa kwenye mfumo ndizo zitakazowezesha ukadiriaji wa kodi.

Akizungumzia mfumo wa TANCIS, Kamishna wa Forodha, Juma Hassan Bakari, alisema umeboreshwa na kuongeza taasisi nyingi zaidi ukiwamo Wakala wa Barabara (TANROAD), viwanja vya ndege na ofisi za mipaka ya nchi, ili kuwarahisishia wafanyabiashara huduma.

Kuhusu maazimio nane, Kamishna Mwenda alisema mamlaka hiyo inalenga kukusanya Sh. trilioni 30.04 katika mwaka huu wa fedha 2024/2025; na kwamba wanakuhamasisha ulipaji wa kodi wa hiari, kuanza kutumia mifumo iliyoboreshwa, kuimarisha uhusiano wake na walipakodi na matumizi ya EFD.

Mengine ni kuweka mazingira sawa ya biashara kwa kuweka mifumo ya haki na sawa ya utozaji wa kodi, kushirikiana na timu iliyoindwa na Rais Samia ya kufanya mapitio ya kodi, kuimarisha huduma kwa walipakodi na vitengo vya ukaguzi na uchunguzi wa kodi ili kuzuia ukwepaji wa kodi.