MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu(THRDC) waliomba Jeshi la Polisi kuacha kuwakamata na kutishia wananchi wa Loliondo wanaotoa maoni yao dhidi ya tume zilizoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni.
THRDC inalaani vikali vitendo vinavyoendelea huko Loliondo vya kukamatwa kwa baadhi wa wananchi wanaotoa maoni yao kuhusiana na tume hizo katika kuunga mkono juhudi za Rais na kutoa mapendekezo kuhusiana na tume hizo.
Onesmo Olengurumwa, Mratibu Kitaifa wa THRDC amesema vitendo vya kukamatwa wananchi na baadhi ya viongozi waliotoa maoni na mitazamo yao kuhusiana na tume hizo ni uvunjifu wa haki za binadamu dhidi ya wananchi wanaotumia haki zao za msingi za kikatiba kutoa maoni yao.
Amesema kupongeza juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kuunda tume mbalimbali na kukosoa muundo wa tume, kushauri na kutoa mapendekezo namna bora ya kuboresha tume hizo ni haki yao ya msingi kwakuwa mambo yanayowagusa moja kwa moja katika mustakabali wa maisha yao.
THRDC inalaani kuona baadhi ya wananchi, na baadhi ya viongozi wa kijamii wa wanawake Loliondo, aliyekuwa Mwenyekiti Mstaafu Wilaya Ngorongoro kuitwa kituo cha Polisi na kuwekwa ndani kwa muda mchache hiyo inaonyesha ni ishara ya vitisho dhidi ya wananchi hao.
“Sisi kama Watetezi wa Haki za Binadamu haturidhishwi na vitendo hivyo, hatutaki kuona wananchi wafungwe macho na masikio wasitoe maoni yao tunaomba vyombo vinavyohusika viache mara moja vitendo hivyo kwakuwa vinawanyima Uhuru na haki kama Watanzania” amesema
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED