MBUNGE wa Jimbo la Mpanda Mjini, Sebastian Kapufi, wamewashauri viongozi wa kisiasa wakiwamo wabunge, wenyeviti wa halmashauri na madiwani kutokuwa sehemu ya washiriki wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya halmashauri husika.
Amesema kufanya hivyo, kunaathiri utekelezaji wa miradi hiyo na thamani ya fedha iliyotolewa inashindwa kuonekana katika miradi inapokamilika.
Kapufi, alisema hayo alipokuwa katika ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua miradi ya maendeleo iliyofanyika katika kata zote za jimbo hilo, lililopo mjini hapa.
Alisema wananchi wanatamani kuona kuna uwiano sawa wa fedha zilizotolewa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo, serikali ikipeleka zaidi ya Sh. bilioni sita, mwaka wa fedha wa 2024/25.
"Mathalani imetolewa Sh. milioni 600 kwenye ujenzi wa mradi wa shule ya sekondari ni vyema hata mwananchi wa kawaida akaona thamani ya mradi huo, ikifanana na fedha zilizotumika sio kuwapo na ujanja ujanja ambao unafanya miradi mingi kutekelezwa chini ya kiwango," alisema.
Alisema viongozi hawapaswi kuwa sehemu ya washiriki katika shughuli hizo, kwakufanya hivyo kutafanya washindwe kutimiza wajibu wao wa kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo.
Hata hivyo, kauli ya Kapufi inakuja wakati ambao viongozi wengi wa kisiasa ni miongoni mwa wamiliki wa makampuni ya ujenzi na wamekuwa wakitajwa kushinda zabuni za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ambayo mingine ikilalamikiwa kutekelezwa chini ya kiwango. Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda, Leonard Kilamhama, alisema serikali imetoa Sh. bilioni 4.7 kwa ajili ya ujenzi wa shule mbili za Shanwe na ya kanda ,itakayochukua wanafunzi kutoka mikoa ya Katavi, Kigoma na Tabora.
Alisema kukamilika kwa ujenzi wa shule hizo kutasaidia kupunguza tatizo la wanafunzi kukosa shule mara wanapofaulu mitihani yao ya mwisho ya kumaliza elimu ya msingi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED