Lissu ataja mambo 7 kuufanya uchaguzi CHADEMA kuwa huru

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 09:59 AM Jan 02 2025
Tundu Lissu.
Picha: Mtandao
Tundu Lissu.

JOTO la uchaguzi wa nafasi ya uenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) likiongezeka, mgombea wa nafasi hiyo, Tundu Lissu amependekeza mambo saba yanayopaswa kufanyika ili uchaguzi huo uwe huru na haki.

Baadhi ya mapendekezo hayo ni kualikwa viongozi wa dini, mabalozi kutoka nchi jirani ambao watakuwa waangalizi pamoja na kura kuhesabiwa mchana. 

Amesema mapendekezo hayo yakifanyika ipasavyo yatasaidia kuondoa mianya ya rushwa, kudhibiti watu wenye nia ovu ya kuvuruga uchaguzi.

Aliyasema hayo jana wakati akitoa salamu za mwaka mpya 2025 kwa wanachama wa chama hicho na Watanzania.

Ameunga mkono hoja ya kuwa na uchaguzi huru na wa haki ndani ya chama, kinyume na hapo hakitoweza kutekeleza kivitendo matakwa ya kikatiba ya kutengeneza uongozi unaoweza kumilikiwa, kuhojiwa na kumilikishwa na umma.

VIONGOZI WA DINI, MABALOZI

Alisema ili uchaguzi huo uwe huru na wa haki, alipendekeza Kamati Kuu ya chama iwaalike viongozi wa dini kama wageni waalikwa na watazamaji ili kuzuia watu waovu kuvuruga uchaguzi huo.

Alisema amependekeza suala hilo kwa sababu chama hicho kina upungufu wa wazee wastaafu ambao katiba inaelekeza wachaguliwe na kamati za chama kwa ajili ya kusimamia uchaguzi huo.

Pia, alishauri Kamati Kuu kuwaalika mabalozi wa nchi jirani ambao ni rafiki ili kuongeza uzito wa uchaguzi na kuongeza macho dhidi ya waliopanga kuharibu uchaguzi huo.

MATUMIZI YA FEDHA

Alitaja pendekezo lingine kuwa ni kamati ya wazee wastaafu wa chama kwa kushirikiana na Ofisi ya Katibu Mkuu kuhakikisha kuwa fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya usafiri wa wajumbe wa vikao vya uchaguzi zitumike kukodisha mabasi au usafiri mwingine utakaowasafirisha kutoka maeneo yao hadi Dar es Salaam na kuwarudisha.

Alipendekeza fedha zilizotengwa kwa ajili ya malazi ya wajumbe zitumike kukodi nyumba za kulaza wageni watakazotumia katika kipindi chote watakapohudhuria vikao vya uchaguzi.

Alisema na fedha za chakula na mambo mengine zilipwe kwa wajumbe watakapowasili jijini.

Kadhalika, alisema mwaka 2012 chama hicho kilitengeneza miongozo ya uchaguzi ambayo pamoja na mambo mengine inazuia utoaji wa rushwa katika uchaguzi, ikiwamo kutoa fedha, chakula, zawadi, au rushwa ya ngono kwa wajumbe au wapigakura kwa lengo la kujipatia fedha.

Aliwasihi wajumbe wa timu yake ya kampeni, vongozi wa wanachama na wafuasi wake kuchukua tahadhari kulinda maisha na usalama wao na kuepuka vishawishi vya kuwa chanzo cha vurugu.

KURA KUHESABIWA MCHANA

Alipendekeza Kamati ya Wazee Wastaafu watakaoteuliwa kusimamia uchaguzi kuhakikisha kuwa kura zinahesabiwa mchana ili kuepuka watu wenye nia mbaya kutumia giza kuleta vurugu na kuharibu uchaguzi.

KUTANGAZA MATOKEO

Alipendekeza shughuli yote ya kupiga na kuhesabu kura na kutangaza matokeo ya uchaguzi ifanyike kwa uwazi mbele ya wajumbe wa mkutano ili kuondoa uwezekano wa kuingiza kura haramu au kubadili matokeo.

WAPIGAKURA

Alishauri watakaoruhusiwa kuingia katika mkutano ni wajumbe, waalikwa na wahudumu maalumu wenye vitambulisho na wagombea au mawakala wao wanashirikishwa katika hatua zote za maandalizi ya mkutano.

Pamoja na mambo mengine, Lissu alishangazwa na mapokeo tofauti ya baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho kuhusu mapendekezo ya ukomo wa madaraka, akisema linaloonyesha kuwa wana lengo la kuirudisha nchi nyuma kikatiba kwa zaidi ya miaka 40.

Aidha, anashangazwa na maoni ya baadhi ya viongozi hao kuwa hoja ya ukomo wa madaraka haifai kutekelezwa ndani ya vyama vya siasa hasa vya upinzani kwa sababu uongozi wake hauna malipo.

“Hoja hii inapaswa kuangaliwa kwa tahadhari kubwa, kama lengo la ukomo wa madaraka ni kudhibiti ving’ang’anizi wa madaraka na kuhakikisha utaratibu wa kuachiana madaraka kwa njia za kikatiba, ukomo wa madaraka unawahusu viongozi wote wa kisiasa bila kujali wanajitolea au wanalipwa mishahara,” alisema.

Alisema tangu nchi iingie kwenye mfumo wa vyama vingi, ni viongozi wa vyama vya upinzani pekee ndiyo wameng’ang’ania madarakani kwa muda mrefu zaidi jambo linalowatia doa katika harakati zao za kudai mfumo bora wa kidemokrasia katika uchaguzi na utawala wa nchi.

Alisema hali hiyo pia imesababisha nafasi za uwakilishi wa viti maalumu katika ubunge na udiwani kuwa za watu wachache, wanaojijengea himaya za kimalkia ndani ya vyama vyao kwa kutumia mafao yao kuendelea kubaki katika nafasi hizo.

Kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Lissu alisema unapaswa kutoa mafunzo kwa ajili ya ustawi wa demokrasia, utawala bora na uwajibikaji katika chama hicho (CHADEMA) na taifa kwa ujumla.

“Tutapiga kura huku tukijua kuwa wapigakura feki wataandikishwa, wagombea wao wataenguliwa, vurugu kwenye kampeni na siku ya uchaguzi, kura halali zitaibiwa, kura feki zitaingizwa na wagombea walioshindwa watatangazwa washindi wa uchaguzi hizo,” alisema.

Alisema kuanzia sasa msimamo wa CHADEMA unatakiwa kuwa ‘bila mabadiliko hakuna uchaguzi’ na itawezekana tu kama kukiwa na uongozi mpya, mbinu mpya na fikra mpya za mapambano ya kidemokrasia.

Alisema baada ya miaka 21 madarakani kwa uongozi uliopita katika chama hicho wasidanganyane kuwa miaka mitano ijayo utaleta mambo mapya ambayo hawajayaona.

Lissu alisema mwaka 2024 uligubikwa na matukio ambayo hayakuwa mazuri kwa chama hicho, yakiwamo ya kutekwa, kuteswa na kuuawa kwa viongozi na wanachama wa chama hicho.