WAKATI Watanzania wakisherehekea Sikukuu ya Mwaka Mpya, viongozi wa dini wametumia mkesha kutoa angalizo kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka huu pamoja na kudumisha amani.
Kwa nyakati tofauti viongozi hao pia wamewakumbusha Watanzania mwaka 2025 kutenda haki pamoja na kusaidia wasiojiweza.
Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kijitonyama, Dk. Eliona Kimaro, alizitaka mamlaka zinazohusika na uchaguzi mkuu mwaka huu kutenda haki kwa vyama vyote, ili kulinda amani ya nchi.
Akihubiri katika moja ya ibada kanisani hapo, Kimaro, alisema hakutakuwa na muujiza wa amani kama haki haitatendeka kwa vyama vyote vya siasa katika uchaguzi huo.
“Mwakani (2025) tunaenda kwenye Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani. Lakini, hamasa tunayohamasisha nchi yetu ni kutenda haki, uchaguzi wa haki ili amani iendelee kuwapo katika nchi yetu,” alisema.
Alisema endapo hakutatendeka haki kuna hatari ya kuhatarisha amani ya nchi, ni bora hilo likazingatiwa kwenye uchaguzi huo.
Alisisitiza kuwa amani ni matokeo ya kazi ya nguvu ya haki ambayo haiji bure bali inatafutwa.
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga, Mhashamu Liberatus Sangu, akihutubia kwenye mkesha wa kuukaribisha mwaka mpya 2025, uliofanyika katika Kanisa Katoliki la Ngokolo Mjini Shinyanga aliwasihi Watanzania kuombea nchi ili iendelee kuwa na amani.
Kadhalika aliwasihi kuwaombea viongozi wenye dhamana ya kuliongoza taifa waweze kuliongoza vyema, bila kusababisha vurugu wala uvunjifu wa amani iliyopo.
Shekhe wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke alisema kwa mwaka huu wa uchaguzi, Tanzania bila kung’angania amani haiwezi ‘kutoboa’ kwa namna yoyote, ni jukumu la kila Mtanzania kutumia nafasi yake kuidumisha.
Mchungaji wa Kanisa la Anglikana Mwanza, Edward Kibiti alisema ni muhimu kuomba ili kupata watu sahihi wa kuliongoza taifa.
Padri George Nzungu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mwanza, alisema ni wakati wa Watanzania kusimama katika Zaburi ya 127 na kuwa asiyeijenga nyumba yake juu ya mwamba huiharibu mwenyewe.
Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi, Ludovick Minde, alisema imefika wakati wa kila mtu kuacha ya ulimwengu na kutafuta suluhisho la kudumu kwa Mungu ili kuepuka matatizo yanayojitokeza kwenye jamii.
Alisema mwaka 2025 ni mwaka wa matumaini kwa kila mmoja atakayemtegemea Mungu na kufanya matendo yaliyomema kwa wenzake.
Askofu wa Jimbo Katoliki la Kahama mkoani Shinyanga, Mhashamu Christopher Ndizeye alisema baada ya kupata madaraka ya uongozi wa udiwani na ubunge wanarudi kanisani kuungama, hivyo mambo hayo wanatenda makusudi kwa uchu wa madaraka.
Alisema, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa baadhi ya maeneo ulighubikwa na vurugu zilizosababisha kuwapo kwa uvunjifu wa amani na baadhi ya wananchi walipoteza maisha na kuishauri serikali kutatua changamaoto zilizojitokeza kabla ya kuingia kwenye uchaguzi mkuu.
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, Wilbroad Kibozi, aliwataka Watanzania kuweka mikakati ya kusaidia watu wasiojiweza, ili waweze kupiga hatua katika shughuli wanazofanya.
Alisema hayo wakati wa maadhimisho ya misa takatifu ya mkesha wa mwaka mpya iliofanyika katika Kanisa Kuu Katoliki la Paulo wa Msalaba Jimbo Kuu la Dodoma.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Karmeli Assembleis of God Tanzania Dk. Evance Chande, alisema kwenye Uchaguzi Mkuu 2025, Watanzania wasikubali kuwachagua wagombea wanaojihusisha na vitendo vya kishirikina na watakao tumia rushwa kutaka kuingia madarakani.
Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Ng'ambo ya Mto Pangani, Warehema Chamshana amesema mwaka huu ni wa Uchaguzi Mkuu, hivyo Watanzania waendelee kuomba kutokana na kwamba ni jambo kubwa kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi.
Pia, aliwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari la Wapigakura ili kuweza kupata ridhaa ya kuwachagua viongozi ambao watawaongoza katika kipindi cha miaka mingine mitano.
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbulu, Antony Lagwen, amewaonya viongozi wenye uchu wa madaraka na mali kuacha kwa kuwa ndicho chanzo cha kupotea kwa amani, huku akiwatwisha mzigo wasomi kutetea haki za watu.
Alisema mara nyingi amani inapokosekana binadamu wenye uchu wa madaraka na uchu wa mali ndiyo hutumia nafasi hiyo.
Pia, alitumia fursa hiyo kuwataka wasomi kusaidia watu kujua haki zao na kutetea haki za wananchi ili watu wazitambue.
*Imeandaliwa na Elizabeth Zaya (Dar), Mary Mosha (Moshi), Shabani Njia (Kahama), Renatha Msungu (Dodoma), Peter Mkwavila (Dodoma), Osca Asenga (Tanga), Jaliwason Jasson (Manyara). Marco Maduhu (Shinyanga), Rose Jacob na Vitus Audax (Mwanza)
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED