INEC yawapa onyo mawakala, viongozi wa siasa

By Gideon Mwakanosya , Nipashe
Published at 11:50 AM Jan 02 2025
Mwenyekiti wa INEC, Jaji mstaafu Jacobs Mwambegele,
Picha:INEC
Mwenyekiti wa INEC, Jaji mstaafu Jacobs Mwambegele,

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewataka mawakala na viongozi wa vyama vya siasa kutoingilia mchakato wa uboreshaji wa Daftari la Wapigakura.

Imewaomba kuzingatia Sheria ya Uchaguzi, kanuni za uboreshaji, maelekezo ya INEC ya kusimamia miiko na mipaka ya uendeshaji wa zoezi hilo.

Mwenyekiti wa INEC, Jaji mstaafu Jacobs Mwambegele, alitoa tahadhari hiyo katika mkutano ulioshirikisha viongozi wa INEC na wadau wa uchaguzi mkoani Ruvuma, hotuba yake ikisomwa na Mkurugenzi wa Daftari na TEHAMA wa INEC, Stanslaus Mwita.

Jaji Mwambegele alisema iwapo kutatokea changamoto ni vyema kukafuatwa sheria na taratibu zilizoainishwa katika sheria zinazosimamia uchaguzi au kuziwasilisha kwa tume kwa ajili ya kuzipatia ufumbuzi.

Pia, aliwaomba kutoa taarifa sahihi na kwa wakati kwa wananchi kuhusu uboreshaji wa Daftari la Mpigakura na kuwahamasisha wananchi wenye sifa wajitokeze kwa wingi.

Alisema INEC imeanza maandalizi ya mzunguko wa tisa kati ya mizunguko 13 ya uboreshaji wa daftari na utahusisha mikoa minne ya Ruvuma kwenye Halmashauri ya Wilaya Mbinga, Halmashauri ya Mji Mbinga na Halmashauri ya Wilaya Songea.

Alisema uboreshaji huo kama ulivyokuwa kwa mwaka 2015 na 2020 utahusisha matumizi ya BVR.

Kwa mujibu wa Jaji Mwambegele, mfumo huo unatumika katika kutambua mtu na kumtofautisha kwa kuwa unahusisha uchukuaji wa alama za vidole vya mikono, picha na saini ambazo zitahifadhiwa kwenye kanzidata.

Mratibu wa Uandikishaji wa Daftari la Wapigakura katika Mkoa wa Ruvuma, Salum Kateula, alisema katika mkoa huo kutakuwa na awamu mbili za uandikishaji.

Awamu ya kwanza itahusisha halmashauri za wilaya tano ambazo ni Manispaa ya Songea, Halmashauri ya Wilaya Songea, Halmashauri ya Wilaya Mbinga, Nyasa na Mbinga mji.

Awamu ya pili itahusisha halmashauri tatu za Tunduru, Namtumbo na Nyasa.

Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania Doyasisi ya Ruvuma, Raphael Haule, aliipongeza INEC kwa kuendesha utaratibu huo ambao utasaidia wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu uboreshaji wa daftari.