Kenya, Tanzania wafunga mwaka kwa ujirani mwema

By Ambrose Wantaigwa , Nipashe
Published at 10:40 AM Jan 02 2025
Kenya, Tanzania wafunga mwaka kwa ujirani mwema.
Picha: Mtandao
Kenya, Tanzania wafunga mwaka kwa ujirani mwema.

MBUNGE wa Jimbo la Kurya Magharibi nchini Kenya, Mathias Rhobi, amesema amani na usalama katika nchi ya Tanzania ni mfano wa kuigwa katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Aliambatana na viongozi wenzake kuhudhuria hafla ya kufunga mwaka ya ujirani mwema iliyoandaliwa na wazee na viongozi kutoka pande zote (Kenya na Tanzania), mjini Tarime.

"Ninashukuru wenzangu kutoka Tanzania kuendelea kuimarisha amani na usalama katika nchi yao hatua ambayo inasababisha nchi zote jirani kuwa salama na kuzuia uhalifu katika maeneo ya mipakani," alisema.

Alisema Tanzania imeweza kubadilisha uongozi awamu sita kwa njia za amani kupitia uchaguzi unaofanyika bila vurugu na uharibifu wa mali.

Viongozi hao walijadiliana kuhusu namna ya kuepuka migawanyiko ya kikanda na vurugu wakati wa uchaguzi na mbinu za kuzuia uhalifu wa mipakani.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Edward Gowele, alisisitiza umuhimu wa wanasiasa kushirikiana kuimarisha usalama kwa kuwa ndio msingi wa kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi.

"Wanasiasa wa pande zote wanapaswa kutumia nafasi zao kuhubiri amani na utengamano kwa kuwa ndio msingi wa kuwezesha serikali yoyote kutekeleza miradi ya kuboresha maisha ya watu wake," alisema.

Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Mara, Esther Matiko (CHADEMA), alisema mikakati ya kuimarisha ulinzi na usalama katika eneo hilo halina itikadi ya vyama na kuwataka wananchi kuepuka migawanyiko kutokana na itikadi zao.